Hamia kwenye habari

FEBRUARI 20, 2019
PUERTO RIKO

Kazi ya Muda Mrefu ya Kutoa Msaada Nchini Puerto Riko Yakamilika

Mashahidi wa Yehova walimaliza rasmi kazi kubwa ya kutoa msaada nchini Puerto Riko Septemba 2018, mwaka mmoja baada ya Kimbunga Irma na Maria kusababisha uharibifu kisiwani humo. Maelfu ya wajitoleaji kutoka kotekote katika eneo la ofisi ya tawi ya Marekani walihusika katika mradi huo wa kutoa msaada.

Halmashauri ya Kutoa Misaada iliyoanzishwa na ofisi ya tawi ya Marekani, ilipanga kazi ya wahubiri 10,000 nchini Puerto Riko waliosaidia kutoa msaada. Ndugu na dada wengine 8,000 kutoka maeneo ya mbali ya Alaska, Bahamas, na Hawaii, walijitolea pia kusaidia kazi hiyo.

Kikundi cha wajitoleaji kumi kilichosaidia katika kutoa msaada nchini Puerto Riko.

Kazi ya kutoa msaada ilihusisha kukarabati Majumba 106 ya Ufalme na Majumba 2 ya Kusanyiko yaliyoharibiwa na vimbunga hivyo. Pia, nyumba 783 za ndugu zetu zilikarabatiwa na nyumba nyingine 73 zilijengwa upya. Baadhi ya ndugu walioathiriwa na dhoruba hizo walipata msaada kupitia serikali au bima ya nyumba.

Wajitoleaji wa ujenzi wakijenga upya nyumba iliyoharibiwa huko Lajas.

Lorne Kowert, ambaye anatumikia katika Dawati la Kutoa Msaada katika ofisi ya tawi ya Marekani, anasema: “Sasa kazi imekamilika, kumbukumbu za kile kilichotimizwa zitaendelea kuimarisha ndugu zetu walioathiriwa na dhoruba, na pia wale waliosaidia kazi ya kujenga upya.”

Picha za nyumba ya dada huko Lares zikionyesha ukarabati uliofanywa.

Pamoja na ndugu na dada zetu nchini Puerto Riko, tunathamini jinsi Yehova anavyotutunza kupitia undugu wa ulimwenguni pote.—1 Petro 5:7.