MEXICO CITY—Desemba 4, 2017, umati wa watu katika mji mdogo wa Tuxpan de Bolaños ulio kwenye eneo la mlimani la Jalisco, Mexico, uliwashambulia ndugu zetu 12 wa jamii ya eneo hilo la Huichol na watu wengine 36 wanaoshirikiana nao, na kuwafukuza kutoka katika nyumba zao. Watu waliofanya shambulizi hilo walikasirika kwa sababu Mashahidi hawashiriki katika tamaduni za kidini za jamii ya Huichol. Kwa kuwa wamenyanyaswa, ndugu zetu wamekata rufaa kwa wenye mamlaka kisheria ili wapate kitulizo.

Mali za ndugu zetu ziliibiwa au kutupwa nje.

Wenye mamlaka nchini Mexico wanaheshimu utamaduni wa jamii ya Huichol hivi kwamba wamewaruhusu kujitawala kwa kiwango fulani. Washambuliaji hao, waliotumwa na serikali ya kitamaduni ya Huichol, waliwatoa kwa jeuri ndugu zetu kutoka nyumbani kwao na baada ya hapo wakazipora na kuiba milango, madirisha, na paa. Vitu vyote ambavyo havikuibwa, vilitupwa ndani ya shimo. Kisha akina ndugu walipelekwa msituni na kuambiwa kwamba wangeuawa ikiwa wangejaribu kurudi.

Mashahidi wa Yehova wa Huichol wakiwa nje ya Jumba la Ufalme.

Mwakilishi wa ofisi ya tawi ya Mexico alisafiri kuonana na waliofukuzwa ili kuwategemeza kiroho na kupanga wapate makao. Wawakilishi wa kisheria wa Mashahidi wa Yehova walikutana na msimamizi wa serikali ya Jalisco, mwendesha-mashtaka wa haki za kibinadamu, mwendesha-mashtaka wa eneo hilo, na msimamizi wa masuala ya waathiriwa wa uhalifu. Mamlaka hizo za kisheria sasa zinafanya uchunguzi kuhusu uhalifu huo.

Ndugu Gamaliel Camarillo, msemaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Mexico, anaeleza hivi: “Tunasikitika sana kwamba waabudu wenzetu, wanaoishi kwa amani katika jamii yao na kuheshimu utamaduni wao, wameshambuliwa kwa sababu tu ya kukataa kushiriki ibada inayosumbua dhamiri zao. Tunatumaini kwamba wenye mamlaka watashughulikia haraka mnyanyaso huo uliochochewa na dini.”

Tunasali kwa ajili ya ndugu zetu ambao wamepoteza makao na mali zao, na tuna uhakika kwamba Yehova ataendelea kuandaa msaada unaohitajiwa kupitia tengenezo lake.—Isaya 32:2.

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

David A. Semonian, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1-845-524-3000

Mexico: Gamaliel Camarillo, simu +52-555-133-3048