Hamia kwenye habari

SEPTEMBA 14, 2017
MAREKANI

Mashahidi Nchini Marekani Wanakabiliana na Kimbunga Harvey

Mashahidi Nchini Marekani Wanakabiliana na Kimbunga Harvey

Habari za karibuni zaidi: Tumesikitika kupata ripoti kwamba dada mmoja aliyezeeka alikufa kwa sababu ya Kimbunga Harvey.

NEW YORK—Kimbunga Harvey kilipiga jiji la ufuoni la Rockport, Texas. Kimbunga hicho kikubwa sana kilipiga siku ya Ijumaa, Agosti 25, 2017. Kufikia Jumapili, kimbunga hicho kilikuwa kimepungua nguvu na kuwa dhoruba ya kitropiki lakini kiliendelea kuharibu eneo la kusini mashariki ya Texas siku ya Jumatano, Agosti 30. Ofisi ya tawi nchini Marekani imepokea habari kuhusu jinsi ndugu na dada zetu walivyoathiriwa na uharibifu uliosababishwa na kimbunga hicho.

Mashahidi 84,000 hivi wanaishi katika eneo lilioathiriwa na kimbunga hicho. Ndugu tisa walijeruhiwa na watano wamelazwa hospitalini. Mashahidi 5,566 wamelazimika kuhama nyumbani kwao. Dhoruba iliharibu nyumba 475 za ndugu zetu; na nyumba 1,182 zinahitaji kufanyiwa marekebisho machache.

Jitihada za wenyeji kutoa msaada zinasimamiwa na waangalizi wa mzunguko katika maeneo ya Austin, Dallas, na San Antonio. Mamia ya ndugu katika majiji hayo wamewakaribisha ndugu zao kutoka Houston na Texas Gulf Coast. Wengine wametoa mchango wa tani 300 za chakula, maji, na vifaa kwa walio na uhitaji.—Methali 3:27; Waebrania 13:1, 2.

Waangalizi wa mzunguko wanaripoti kwamba makutaniko yote yamerudia ratiba za kawaida za mambo ya kiroho. Washiriki wa Halmashauri ya Tawi ya Marekani wanapanga kutembelea maeneo yaliyoathiriwa ili kuandaa faraja na kuwategemeza.

“Tunawasikitikia sana wote wanaoteseka kwa sababu ya matokeo ya Kimbunga Harvey, na tunawashukuru wote waliojitolea kusaidia wakati wa majanga hayo,” anasema David A. Semonian, msemaji wa Mashahidi wa Yehova. “Tungependa hasa kuwakumbuka katika sala ndugu na dada zetu walioathiriwa na dhoruba hiyo. Pia, tunawahimiza waendelee kutegemea mkono wa Yehova uwategemeze.”—Zaburi 55:8, 22; Isaya 33:2; 40:11.

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

David A. Semonian, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1-845-524-3000