Kwa miaka 65 hivi, vijana Wakristo nchini Korea Kusini wamekuwa wakifungwa gerezani kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Alhamisi, Juni 28, 2018, uamuzi wa muhimu sana wa Mahakama ya Kikatiba ulibadili hali hiyo kwa kutangaza kwamba Kifungu cha 5, sehemu ya 1, ya Sheria ya Utumishi wa Kijeshi haupatani na katiba kwa sababu serikali haijatoa utumishi badala wa kiraia.

Wanahabari wakiwa nje ya Mahakama ya Kikatiba. Kesi hiyo ilifuatiliwa kwa ukaribu na wanahabari wa kimataifa.

Kikundi cha mahakimu tisa kilichoongozwa na Jaji Mkuu Lee Jin-sung, kilitangaza uamuzi ulioungwa mkono na majaji 6 dhidi ya 3. Uamuzi huo utafanya nchi hiyo ipatane na viwango vya kimataifa na kutambua uhuru wa dhamiri, kufikiri, na imani.

Wawakilishi wa Mashahidi wa Yehova nchini Korea wakiwa ndani ya Mahakama ya Kikatiba muda mfupi kabla ya uamuzi kutolewa.

Korea Kusini imekuwa ikiwafunga gerezani watu wengi zaidi kila mwaka kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri kuliko nchi nyingine zote. Wakati fulani, ndugu zetu 500 hadi 600 hivi walifungwa gerezani kila mwaka. Baada ya kuachiliwa huru, ndugu hao wote walipata shida maisha yao yote kwa sababu ya kuwa na rekodi ya kufungwa, kwa hiyo walikabili changamoto mbalimbali kutia ndani kutopata ajira.

Hata hivyo, kuanzia mwaka wa 2011, ndugu fulani walituma malalamiko kwenye Mahakama ya Kikatiba kwa sababu sheria haikutoa utumishi wa badala, na wote waliokataa utumishi wa kijeshi walifungwa gerezani. Vivyo hivyo, tangu mwaka wa 2012, hata mahakimu waliotatizwa na zoea la kuwaadhibu wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri waliamua kuahirisha kesi ili kusubiri uamuzi ufanywe na Mahakama ya Kikatiba ili Sheria ya Utumishi wa Kijeshi ichunguzwe tena.

Hong Dae-il, msemaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Korea, akihojiwa nje ya mahakama baada ya uamuzi huo

Jukumu la Mahakama ya Kikatiba ni kuchunguza ikiwa sheria fulani inapatana na Katiba ya Korea au la. Baada ya kutoa uamuzi uliounga mkono Sheria ya Utumishi wa Kijeshi (mwaka wa 2004 na 2011), mwishowe mahakama hiyo imekubali kwamba mabadiliko yalihitaji kufanywa. Mahakama imeagiza serikali ya Korea Kusini iandike upya sheria hiyo ili kuwe na utumishi wa badala kufikia mwishoni mwa mwaka wa 2019. Utumishi wa badala unaweza kutia ndani kufanya kazi hospitalini na huduma nyingine zisizohusisha jeshi ambazo zinaweza kuchangia kuboresha jamii.

Ili kutusaidia kuelewa umuhimu wa uamuzi huo, Ndugu Hong Dae-il, msemaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Korea, alisema hivi: “Mahakama ya Kikatiba ambayo ni mahakama yenye nguvu zaidi nchini ndiyo inayopaswa kulinda kabisa haki za kibinadamu, imeandaa msingi wa kutatua suala hili. Ndugu zetu wanatazamia kwa hamu kuhudumia jamii yao kupitia utumishi wa badala wa kiraia ambao haupingani na dhamiri yao na unaopatana na viwango vya kimataifa.”

Masuala mengine muhimu yanahitaji kutatuliwa, yanatia ndani Mashahidi 192 walio gerezani sasa na kesi za uhalifu 900 hivi ambazo hazijashughulikiwa mahakamani.

Uamuzi wa kihistoria wa Mahakama ya Kikatiba inaandaa msingi thabiti wa Mahakama Kuu kutoa uamuzi mzuri katika kesi kuhusu watu mmoja-mmoja wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Uamuzi wa majaji wote wa Mahakama Kuu utaathiri jinsi kesi hizo za uhalifu zitakavyoshughulikiwa.

Mahakama Kuu inatarajiwa kusikiliza mkutano wa umma Agosti 30, 2018 kwa ajili ya pendekezo hilo, na itatoa uamuzi wake muda fulani baadaye. Itakuwa mara ya kwanza katika miaka 14 ambapo majaji wote wa Mahakama Kuu watazungumzia suala la kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.

Wakati huohuo, bunge la Korea tayari limeanza mipango ya kurekebisha Sheria ya Utumishi wa Kijeshi.

Ndugu Mark Sanderson wa Baraza Linaloongoza anasema hivi: “Tunatarajia kwa hamu kusikia uamuzi wa Mahakama Kuu. Ndugu zetu nchini Korea wamedhabihu kwa hiari uhuru wao, wakijua kwamba “inakubalika ikiwa mtu anavumilia taabu na kuteseka isivyo haki kwa sababu ya dhamiri kwa Mungu.” (1 Petro 2:19) Tunashangilia pamoja nao kwamba ukosefu huo wa haki umetambuliwa, na tunathamini msimamo wa dhamiri yao unaoonyesha ujasiri.”