Hamia kwenye habari

MEI 7, 2018
KOREA KUSINI

Mashahidi wa Yehova Watumia Vigari Kusambaza Machapisho Wakati wa Michezo ya 2018 ya Olimpiki na Olimpiki ya Walemavu

Wakati wa Michezo ya Olimpiki na Olimpiki ya Walemavu ya Pyeongchang ya 2018 ya Majira ya Baridi Kali, iliyofanyika Februari 9-25, 2018, na Machi 9-18, 2018, ndugu na dada nchini Korea walikuwa na kampeni ya pekee ya kuwapa wageni wengi wa kimataifa machapisho ya Biblia bila malipo.

Ndugu na dada zaidi ya 7,100 kotekote nchini walishiriki kampeni hiyo. Wengi wao walitoka majiji ya Busan, Gwangju, Incheon, Seoul, na Suwon; baadhi hata walitoka mbali kwenye Kisiwa cha Jeju, eneo linalopendwa na watalii kilomita zaidi ya 480 hivi kusini ya Pyeongchang.

Ndugu zetu walisimamisha vigari 152 vya hadharani katika maeneo 48, kutia ndani Uwanja wa Olimpiki wa Gangneung na Jengo la Pyeongchang la Olimpiki. Pia waliruhusiwa kuweka machapisho kwenye mwingilio mmoja wa vituo vya kidini vya Kijiji cha Olimpiki.

Vigari viwili karibu na lango la kaskazini la Uwanja wa Olimpiki wa Gangneung.

Pia, wenye mamlaka waliwaruhusu ndugu zetu kuweka vigari kwenye Stesheni ya Gangneung, kituo cha mwisho katika safari ya mwendo-kasi ya KTX Gyeonggang, inayowasafirisha abiria kutoka Incheon na Seoul hadi Pyeongchang. Siku ya kwanza ya Michezo ya Olimpiki, zaidi ya watu 28,000 walisafiri kupitia Stesheni ya Gangneung.

Ndugu zetu walitayarisha vitabu, broshua, magazeti, na trakti katika lugha kama 20 hivi kutia ndani Kichina, Kiingereza, Kikazakh, Kikorea, na Kirusi kwa ajili ya wageni 80,000 hivi. Isitoshe, ndugu na dada waliojua Lugha ya Ishara ya Kikorea walitumia video za lugha ya ishara kuwakaribisha viziwi wengi waliokuja kwenye Olimpiki ya Walemavu. Machapisho zaidi ya 71,200 yalisambazwa, kutia ndani mialiko 22,000 ya Ukumbusho.

Ulimwenguni pote, Mashahidi wa Yehova wanatumia vigari zaidi ya 300,000 kusambaza machapisho yao katika nchi zaidi ya 35. Kwa njia hiyo, wanaweza kuwafikia watu popote wanapopatikana na kutimiza huduma yao kikamili.—2 Timotheo 4:5.