Hamia kwenye habari

APRILI 2, 2019
KAZAKHSTAN

Mashahidi wa Yehova Nchini Kazakhstan Walikuwa na Siku za Wageni Katika Majumba ya Ufalme

Kuanzia Mei 11 hadi Novemba 10, 2018, Mashahidi wa Yehova nchini Kazakhstan walitenga siku saba za kuwaalika wageni, katika majiji saba tofauti kotekote nchini. Matukio hayo yametokeza fursa kwa maofisa wa serikali, waandishi wa habari, na wasomi, pamoja na watu kwa ujumla kujifunza mengi zaidi kuwahusu Mashahidi wa Yehova. Jumla ya watu waliotembelea majumba hayo ni watu zaidi ya 1,500.

Matukio hayo yalifanyika katika majiji yafuatayo: (1) Öskemen, (2) Qaraghandy, (3) Qostanay, (4) Semey, (5) Shymkent, (6) Taldyqorghan, na (7) Taraz.

Siku hizo za wageni zilifanywa katika Majumba ya Ufalme katika majiji ya Öskemen, Qaraghandy, Qostanay, Semey, Shymkent, Taldyqorghan, na Taraz. Watu waliotembelea majumba hayo walifurahia kuona chati na picha zilizoonyesha historia ya kazi yetu nchini Kazakhstan, ambayo ilianza tangu 1892. Picha hizo zilionyesha pia mambo yaliyotimizwa katika miaka ya karibuni, kama vile kutolewa kwa Biblia Takatifu—Tafsiri ya Ulimwengu Mpya katika Kikazakh mwaka wa 2014.

Ndugu Bekzat Smagulov, anayefanya kazi katika Idara ya Mambo ya Kisheria na Dawati la Habari za Umma kwenye ofisi ya tawi ya Kazakhstan, ametaja faida walizopata: “Majirani wetu waliohudhuria matukio hayo walifurahia kwelikweli, na hilo limewasaidia kupata ujuzi sahihi juu yetu. Miongoni mwa wageni kulikuwa na viongozi wa Idara ya Masuala ya Kidini na waandishi wa habari wa shirika la Kazakhstan-Öskemen, gazeti Rudnyi Altai, na gazeti Semei Vesti.”

Katika mji wa Taldyqorghan, kituo cha usimamizi cha jiji la Almaty, akina ndugu walimkaribisha mkuu wa Idara ya Masuala ya Kidini wa Jiji hilo na maofisi wawili wa idara hiyo. Pia, mhariri mkuu wa gazeti Zhetysu Dialog alihudhuria tukio hilo, na baadaye akaandika makala kadhaa kuhusu kuwahoji wajitoleaji katika tukio hilo.

Kwa kuongezea, ndugu na dada zetu walitoa nakala zaidi ya 560 za Tafsiri ya Ulimwengu Mpya katika Kikazakh na Kirusi, lugha kuu za Kazakhstan. Tunafurahia matokeo mazuri yaliyotokana na mpango huo unaomletea Yehova sifa na kuwapa majirani wetu nafasi ya kuona “matendo [yetu] mema.”— Mathayo 5:16.

 

Jijini Qaraghandy, Dada Saniya Akhmetzhanova akitumia lugha ya alama kuwasiliana na wenzi wa ndoa viziwi waliozuru awaeleza kuhusu jitihada zetu za kutoa elimu ya Biblia kwa viziwi.

Watoto wawili wadogo wakitazama video yenye kichwa Walinde Watoto Wako katika Kirusi kwenye siku ya wageni jijini Qaraghandy.

Ndugu Lev Gladyshev akiwaeleza maofisa wa serikali waliotembelea jumba la Qaraghandy kuhusu historia ya Mashahidi wa Yehova nchini Kazakhstan. Wageni hao walitia ndani karani wa bunge la eneo hilo, Kudaibergen Beksultanov; mtaalamu mkuu wa Idara ya Uchunguzi wa Masuala ya Kidini, Nikolay Sarsenbayev; na mkuu wa Idara ya Masuala ya Kidini wa Jiji la Qaraghandy, Nurlan Bikenov.

Dada Aisha Yakovleva akiwaeleza wenzi wa ndoa walioshiriki siku ya wageni jijini Taldyqorghan mambo yenye kupendeza katika programu ya JW Library®.

Ndugu Aleksey Alyoshin akiwaonyesha wageni katika jiji la Taraz jinsi jina la Mungu lilivyoonekana kwa miaka mingi katika maandishi mengi ya kale na kwenye vitu vilivyochimbuliwa.

Katika siku ya wageni huko Öskemen, Ndugu Sergey Petkevich akiwa ameshika nakala ya zamani ya Mnara wa Mlinzi katika Kirusi, huku akieleza historia ya Mashahidi wa Yehova nchini Kazakhstan. Miongoni mwa wageni walioshiriki siku ya wageni ni mkuu wa shirika la umma la Edinstvo, Sergey Lebedev.

Ndugu Georgiy Pismenoy (upande wa kulia) akizungumza na mmoja wa majirani aliyefika kwa ajili ya siku ya wageni iliyofanyiwa Qostanay. Wageni waliofika walitazama video ya mwaka wa 1982 iliyoonyesha jinsi kesi ilivyoendeshwa mahakamani iliyohusisha ndugu watatu na dada mmoja jijini Qostanay waliohukumiwa kwa kosa la kumiliki, kuchapisha, na kusambaza machapisho yetu ambayo yalikuwa yamepigwa marufuku wakati huo. Ndugu Pismenoy alikuwa mmoja wa ndugu watatu waliohukumiwa kifungo cha miaka miwili na nusu ya kazi ngumu. Alieleza hali aliyokabiliana nayo alipokuwa gerezani.

Wageni walikaribishwa na wanamuziki wakipiga ala zao, kama vile Kazakh dombra (inayoonyeshwa upande wa kushoto kabisa na mwishoni kulia), katika siku ya wageni huko Shymkent.

Ndugu na dada waliojitolea kusaidia katika siku ya wageni jijini Qaraghandy.