Hamia kwenye habari

MACHI 28, 2019
INDONESIA

Mafuriko ya Ghafla Nchini Indonesia

Mvua kubwa zilipiga mkoa wa mashariki wa Papua, nchini Indonesia, Machi 16, 2019. Mvua hizo zilisababisha mafuriko ambayo yameua watu zaidi ya 100 na kusomba nyumba kadhaa.

Ofisi ya tawi ya Indonesia inaripoti kwamba ndugu wengi wanaoishi katika mji wa Sentani, ulio katika mkoa wa Papua, wameathiriwa na janga hilo. Inasikitisha kwamba ndugu yetu mmoja alikufa nyumba yake iliposombwa na mafuriko hayo. Na nyumba nyingine tatu za familia za Mashahidi ziliharibiwa kabisa. Wahubiri zaidi ya 40 wamehamishwa, na wengi wao wanaishi na Mashahidi wenyeji. Halmashauri ya Kutoa Misaada imeanzishwa ili kupanga kazi ya kutoa msaada. Wawakilishi wa ofisi ya tawi, pamoja na mwangalizi wa mzunguko wa eneo hilo, wametembelea maeneo yaliyoathiriwa ili kuandaa faraja ya kiroho. Pia wanakagua eneo hilo ili kujua kiasi cha msaada kinachohitajika.

Tunasali kwa ajili ya ndugu wote walioathiriwa na janga hilo. Tunatamani siku ambayo hivi karibuni Yehova “atameza kifo milele” na “atafuta kabisa machozi katika nyuso zote.”—Isa 25:8.