Hamia kwenye habari

MEI 27, 2020
HISPANIA

Wenzi wa Ndoa Nchini Hispania Wapokea Barua ya Shukrani Kutoka kwa Mhudumu

Wenzi wa Ndoa Nchini Hispania Wapokea Barua ya Shukrani Kutoka kwa Mhudumu

Wakati huu wa ugonjwa wa virusi vya corona, ndugu na dada wengi wanajitahidi kuwafariji majirani kwa kuwaandikia barua zenye kutia moyo. Ndugu Josué Laporta na mke wake, Vanesa, waliandika barua za kuwapa pole wahudumu wa afya na wagonjwa wa virusi vya corona katika hospitali jijini Barcelona, Hispania. Mhudumu mmoja aliwaandikia ili kuwashukuru. Ifuatayo ni barua yake, ambayo alitoa idhini kwamba iwekwe mtandaoni baada ya kuondoa habari fulani. *

Mimi ni mhudumu wa afya (nesi) . . . na ninaandika kwa niaba ya [jina limeondolewa], mama mwenye umri wa miaka 97. Tulimsomea barua yenu leo asubuhi. Wagonjwa hupewa barua na wafanyakazi wa hospitali bila mpangilio wowote, lakini nina hakika kwamba barua hii haikumfikia kwa sadfa tu. Barua hii imewasaidia watu wawili, [mgonjwa] na mimi . . . , kuona kwamba kuna tumaini. Huenda [mgonjwa] hana muda mrefu wa kuishi, naye aliniambia kwamba asingependa kuondoka ulimwenguni bila kukuuliza, Josué, swali hili: “Hata nikiwa na umri wa miaka 97, je, bado ninaweza kufaidika kutokana na ahadi zilizotabiriwa katika Biblia?”

Leo asubuhi nilifaulu kutumia dakika kumi kumsomea [mgonjwa] sehemu fulani ya tovuti uliyonielekeza. Macho yake yaling’aa, akawa na furaha, na uso wake ukawa na shangwe na amani, hajawahi kuhisi hivyo kwa muda aliokuwa hapa. Kisha akatazama video yenye kichwa “Kwa Nini Yesu Alikufa?

Pia nilisoma gazeti [“Amkeni!”] kuhusu mkazo na ikanisaidia kukabiliana na hali yetu ya sasa. Kama mjuavyo, hali yetu si rahisi.

Hakuna wanasaikolojia wa kuzungumza na wafanyakazi wa afya, lakini habari hiyo inapatikana saa 24 kwa siku na tunaweza kutafakari kuihusu. Ugonjwa huu utakapokwisha, ningependa kujua mengi zaidi na ninatumaini kwamba mtakuwepo ili kunifundisha yote ninayohitaji kujua, ili mnihakikishie kwamba kutakuwa na ulimwengu bora zaidi. Sijui niseme nini ili kumshukuru Mungu kwamba barua yenu ilifika siku hiyo, wakati uleule ambao nilikuwa zamu, na kwamba mimi ndiye niliyempelekea [mgonjwa] chumbani mwake.

Ninatumaini kwamba wewe na familia yako ni wazima na mna afya njema, nina hakika kwamba tumaini mlilo nalo linawasaidia kukabiliana na hali ya sasa kwa njia nzuri zaidi kuliko wengi wetu. Asante sana kwa wakati mnaotenga ili kuwasaidia watu kama [mgonjwa] na mimi. Ingawa hatufahamiani, mmetufanya tutabasamu zaidi kuliko ambavyo tumetabasamu katika majuma sita yaliyopita.

Nawashukuru kutoka moyoni.

Maneno kama hayo ya shukrani yanatutia moyo kuendelea kuhubiri hata katika kipindi hiki ambapo ugonjwa unaendelea. Tunasali kwamba maneno tunayochagua kutumia katika huduma, yatawaletea wengine faraja.—Methali 15:23.

^ fu. 2 Barua ya awali iliandikwa katika Kihispania.