Hamia kwenye habari

Picha hii ilipigwa kabla ya kipindi cha ugonjwa wa virusi vya corona. Cynthia (kushoto), mhubiri ambaye hajabatizwa na ambaye pia ni kiziwi na kipofu, anawasiliana na dada katika kutaniko lake kupitia ishara za mkononi

MEI 12, 2020
FILIPINO

Kutaniko Lamsaidia Dada Ambaye Ni Kiziwi na Kipofu Wakati wa Ugonjwa wa Corona

Kutaniko Lamsaidia Dada Ambaye Ni Kiziwi na Kipofu Wakati wa Ugonjwa wa Corona

Dada Cynthia Pablo ni mhubiri ambaye hajabatizwa mwenye umri wa miaka 64 anayehudhuria mikutano katika Kutaniko la Lugha ya Ishara la Panghulo nchini Filipino. Yeye ni kiziwi na kipofu na ni maskini. Anaishi na watu wake wa ukoo katika eneo lenye watu wengi sana katika Jiji la Valenzuela. Ingawa Cynthia ana changamoto nyingi zinazotokezwa na hali yake na ambazo zimeongezeka kwa sababu ya ugonjwa huu, akina ndugu katika kutaniko lake wamekuwa wakimwandalia mahitaji yake.

Akitumia pikipiki yake, Ndugu Ilumin anampelekea Cynthia nguo safi na misaada

Kwa sababu ya umri wake, Cynthia anaweza kuathiriwa kwa urahisi zaidi na ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19). Ugonjwa huo umesababisha ukosefu wa maji katika eneo lake, kwa hiyo imekuwa vigumu kwake kuosha nguo zake. Kabla ya ugonjwa wa corona kutokea, akina dada katika kutaniko lake walikuwa wakimsaidia Cynthia kufanya kazi hiyo, lakini vizuizi vya serikali vimefanya hilo lisiwezekane.

Ndugu Walter Ilumin, mzee wa kutaniko lake, alipata cheti cha pekee kutoka serikalini, kinachompa idhini ya kutoka nyumbani kwake ili kumshughulikia Cynthia. Cheti hicho kinatolewa tu kwa watu wanaotoa huduma za lazima. Mbali na kuosha nguo zake, Walter humletea pia bidhaa nyingine za pekee. Anafuata miongozo ya eneo lao na pia ya serikali, inayotia ndani kuvaa barakoa (mask) na vifaa vingine vya kujilinda na kunawa mikono yake mara nyingi.

Ili kuwashukuru akina ndugu na dada, Cynthia hurekodi video zenye ujumbe mfupi na kuwaeleza jinsi anavyothamini msaada wao. Kisha Ndugu Ilumin huwaonyesha wote kutanikoni video hizo.

Cynthia akishiriki katika kazi ya kuhubiri kabla ya ugonjwa wa virusi vya corona

Mzee huyo husafiri pia kwenda nyumbani kwake ili kumtafsiria mikutano ya kutaniko inayofanywa kupitia video iliyounganishwa kwenye mtandao akitumia ishara mkononi mwake. Kwa sababu hiyo, Cynthia anaweza kutoa maelezo kwa ukawaida wakati wa Funzo la Mnara wa Mlinzi. Anapotoa maelezo mikutanoni wakati wa kipindi hiki kigumu anawatia moyo wengine waliounganishwa.

Tuna uhakika kwamba Yehova anapendezwa kuwaona watu wake wakiandaa faraja na msaada miongoni mwao ‘na wakifanya hivyo zaidi kwa kadiri wanavyoona siku ile ikikaribia.’—Waebrania 10:24, 25.