Hamia kwenye habari

OKTOBA 10, 2018
JAPANI

Trami: Kimbunga Kilichoipiga Japani Karibuni Zaidi

Trami: Kimbunga Kilichoipiga Japani Karibuni Zaidi

Jumapili jioni Septemba 30, 2018, Kimbunga Trami kilipiga eneo la kusini la Japani na kutokeza upepo mkali na mvua kubwa sana. Nguvu za dhoruba hiyo zilipungua kadiri ilivyosonga upande wa kaskazini na hatimaye kufika jijini Tokyo siku ya Jumatatu, Oktoba 1. Watu watatu walikufa, 200 hivi wakajeruhiwa, na umeme ukakatwa katika nyumba zaidi ya milioni 1.3.

Kulingana na ripoti kutoka kwa waangalizi wa mzunguko, kisiwa cha Okinawa, kilichoko Japani kusini, ndicho kilichoathiriwa zaidi. Uchunguzi wa awali kutoka mizunguko mitatu ya Okinawa na maeneo ya karibu unaonyesha kwamba hakuna ndugu aliyekufa lakini tisa walijeruhiwa. Pia kimbunga hicho kiliharibu nyumba 120 hivi za ndugu zetu katika kisiwa cha Okinawa na Majumba 5 ya Ufalme. Majumba mengine 41 ya Ufalme yaliathiriwa kimbunga hicho kilipopita katika maeneo mengine ya Japani.

Waangalizi wa mzunguko wa eneo hilo na washiriki wa Idara ya Usanifu Majengo na Ujenzi wanaendelea kufanya uchunguzi ili kufahamu majengo yaliharibiwa kwa kadiri gani na kuamua ni msaada gani wa kiroho na wa kimwili unaohitajika.

Tunaendelea kusali kwa ajili ya waabudu wenzetu walioathiriwa na kimbunga hiki na misiba mingine ya asili ambayo imetokea hivi karibuni nchini Japani. Tuna uhakika kwamba Baba yetu wa mbinguni ataendelea kuifariji mioyo ya ndugu zetu na kuwaimarisha.—2 Wathesalonike 2:17.