NEW YORK—Kulingana na uchunguzi uliofanyiwa kwenye Chuo Kikuu cha Michigan mwaka wa 2017 na Mott Children’s Hospital National Poll on Children’s Health, wazazi nchini Marekani wanasema kwamba kunyanyaswa kwa watoto shuleni ni mojawapo ya matatizo makubwa zaidi.

Tovuti ya stopbullying.gov, inayosimamiwa na Idara ya Afya na Huduma za Jamii ya Marekani , inafunua huenda ni kwa nini wazazi wanahangaishwa sana: Utafiti unaonyesha kwamba asilimia 30 hivi ya wanafunzi nchini Marekani walisema walikuwa wamenyanyaswa shuleni.

David A. Semonian ambaye ni msemaji wa Mashahidi wa Yehova kwenye makao makuu jijini New York, , alisema hivi: “Tunatambua kwamba watoto wengi wananyanyaswa. Ikiwa sehemu ya kazi yetu ya kufundisha Biblia, tunaandaa vifaa vya kushughulikia unyanyasaji na changamoto nyingine ambazo familia zinakabili. Kwa miaka mitano hivi sasa, familia nyingi ulimwenguni pote zimenufaika sana kutokana na kibonzo kwenye ubao chenye kichwa: Mshinde Mnyanyasaji Bila Kutumia Ngumi.

Picha iliyo katika video Mshinde Mnyanyasaji Bila Kutumia Ngumi, inawatia moyo vijana wanaonyanyaswa wawaambie wazazi, wasimamizi wa shule, au mtu mzima wanayemtumaini.

Video hiyo yenye urefu wa dakika nne tu, inapatikana kwenye tovuti rasmi ya Mashahidi, jw.org, katika lugha zaidi ya 280, kutia ndani lugha zaidi ya 30 za ishara.

“Ninapenda sana wazo la kumshinda mnyanyasaji bila kutumia ngumi,” anasema Natalia Cárdenas Zuluaga, msimamizi wa programu ya Afya ya Kiakili ya Mtoto na Tineja katika Chuo Kikuu cha CES kilicho Kolombia, “kwa sababu katika nchi yetu, mara nyingine wazazi wanawafundisha watoto kutatua matatizo kwa kutumia jeuri. Ninafikiri video hiyo inatoa mapendekezo mazuri yanayoweza kutumiwa na watoto wanaonyanyaswa. Pia, video hiyo inaonyesha ukweli muhimu kuhusu unyanyasaji: Kwamba mtu yeyote anaweza kunyanyaswa kwa sababu anaonekana yuko tofauti na wengine. Kuelewa ukweli huo kunaweza kuwapa watoto amani na uhakika kuhusu maumbile yao na utu wao.”

Dakt. Jun Sung Hong, profesa msaidizi katika Chuo Kikuu cha Sungkyunkwan kilicho Korea Kusini, anasema hivi: “Kwa kuwa inatumia vibonzo, video hiyo itasaidia na pia kufurahisha watoto wadogo wanaonyanyaswa. Pia, ninaona itakuwa rahisi kwa watazamaji kukumbuka kwa sababu ya michoro iliyotumiwa.”

Isitoshe, Dakt. Shelley Hymel, mmoja wa wale walioshiriki kuanzisha Mfumo wa Utafiti wa kimataifa, alisema hivi: “Ninafikiri huo ni ujumbe mzuri kwa watoto na utafiti uliofanywa unalingana na utafiti niliofanya. Inaweza kutumiwa kuanzisha mazungumzo na wazazi, walimu, au watu wazima wanaofanya kazi na watoto na vijana.”

Bw. Semonian anamalizia kwa kusema hivi: “Tunahangaikia watoto wanaonyanyaswa na tunatumaini kwamba watapata madokezo yanayofaa katika video hiyo. Kama video inavyopendekeza, vijana wanapaswa kumweleza hisia mtu wanayemwamini, hasa wazazi wao au mwalimu, ambaye anaweza kumwongoza na kumtegemeza. Hakuna yeyote anayepaswa kushughulikia unyanyasaji akiwa peke yake.”

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

David A. Semonian, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1-845-524-3000