Hamia kwenye habari

Mashahidi wa Yehova

Chagua lugha Kiswahili

FEBRUARI 14, 2017
MAREKANI

Shirika la GBI Latoa Tuzo la Juu Zaidi kwa Sababu ya Majengo Yasiyoharibu Mazingira ya Makao Makuu ya Mashahidi

Shirika la GBI Latoa Tuzo la Juu Zaidi kwa Sababu ya Majengo Yasiyoharibu Mazingira ya Makao Makuu ya Mashahidi

NEW YORK—Baada ya kukamilishwa kwa ujenzi wa makao makuu mapya ya Mashahidi wa Yehova mnamo Agosti 2016, Mashahidi walitambuliwa rasmi kwa sababu ya ujenzi wa majengo yao mapya yasiyoharibu mazingira kule Warwick, New York. Shirika la Majengo Yasiyoharibu Mazingira (GBI), linalohusika katika kukagua na kutoa vyeti kwa majengo yote ya kibiashara ikiwa majengo hayo yanajitahidi kuhifadhi mazingira, liliwapa Mashahidi tuzo la juu zaidi la Four Green Globes kwa ajili ya majengo yote saba yaliyohusika katika ukaguzi huo.

Shania Weinstein, mkurugenzi wa utekelezaji wa GBI, anasema hivi: “Kati ya miradi 965 ya ujenzi nchini kote, ni majengo 64 tu ambayo yamepokea tuzo la juu zaidi la Four Green Globes. Kwa Mashahidi wa Yehova kupokea Four Green Globes kwa ajili ya majengo yote saba ya Warwick ni jambo la ajabu. Jambo hilo linaonyesha kwamba wanazingatia sana utunzaji wa maji, nishati, na mazingira.”

Mfumo wa ukadiriaji wa Four Green Globes, tuliotumiwa na GBI. Majengo yote saba ya Mashahidi yaliyostahili ukaguzi huo yalipata angalau asilimia 90, alama zinazolingana na kupata Four Green Globes.

Kulingana na tovuti yao rasmi, GBI ni “shirika lisilo la kiserikali lililokusudiwa kuchochea mbinu za ujenzi zinazotokeza majengo yanayotumika bila gharama kubwa, salama kwa afya, yanayosaidia kuhifadhi mazingira.” Shirika la GBI linakadiria viwango vya ubora kwa kutegemea jinsi muundo na matumizi ya majengo mapya yanavyosaidia kudumisha mazingira. Kama sehemu ya ukadiriaji huo, mtaalamu ambaye si wa shirika la GBI hufanya ukaguzi wake ili kuthibitisha maoni yaliyotolewa na shirika la GBI.

David Bean, mratibu wa muundo wa ujenzi usioharibu mazingira katika majengo ya Mashahidi nchini Marekani, anasema hivi: “Tunathamini tuzo hizi, ambazo zinathibitisha kazi nyingi iliyohusika katika ujenzi huu ili kutokeza majengo yaliyo na muundo usioharibu mazingira—majengo yanayopatana vizuri na Msitu wa Kitaifa wa Sterling.”

Paa la Jengo la Ofisi na Huduma, lililo na mimea ya eneo hilo iliyopandwa kwenye kisehemu kinachofaa kilicho juu ya utando usioshika maji. Maji ya mvua kutoka kwenye jengo hilo yanasafishwa na kutumiwa kupunguza matumizi ya maji ya umma.

Mbinu ya Mashahidi ilihusisha kudumisha miti iliyopo katika eneo lao na kutumia mbao za miti iliyokatwa katika mradi wa ujenzi. Jeffrey Hutchinson aliyekuwa msimamizi wa Msitu wa Sterling alisema kwamba “nilithamini sana kwamba baada ya kukata miti ili kupata eneo la ujenzi waliamua kutumia mbao za miti hiyo wakati wa ujenzi. Inapendeza sana kuona jinsi ambavyo Mashahidi wametunza mazingira.” Shaina Weinstein pia anasema hivi, “Kwa maoni yetu, ujenzi wa Warwick unaweka kielelezo cha jinsi ujenzi unaozingatia mazingira unavyopaswa kufanywa.”

Richard Devine, mwenyekiti wa Halmashauri ya Mradi wa Ujenzi wa Mashahidi wa Warwick, anaeleza hii: “Kwa miaka mingi, tengenezo letu limedumisha umaridadi wa majengo yetu kule Brooklyn. Sasa tunatazamia kudumisha majengo yasiyoharibu mazingira ya Warwick na kuhifadhi umaridadi uliopo wa Msitu wa Sterling.”

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

David A. Semonian, Ofisi ya Habari za Umma, 1-845-524-3000

 

Majengo ya makao makuu mapya ya ulimwenguni pote ya Mashahidi kule Warwick yako katika eneo lenye ukubwa wa asilimia 20 tu ya uwanja wote wenye ekari 253 ulionunuliwa Julai 17, 2009.

Blanketi za kuzuia mmomonyoko na mawe ya ukubwa mbalimbali yamewekwa ili kuimarisha udongo uliotumiwa katika ujenzi wa barabara.

Mawe makubwa yakiondolewa katika eneo la ujenzi wakati wa awamu za kwanza za ujenzi. Zaidi ya tani 240,000 za mawe ya eneo hilo yalitumiwa tena wakati wa ujenzi.

Ili kulinda udongo wa ziwa la Blue Lake, ukuta wa aina fulani ulijengwa karibu na ufuo. Sehemu ya juu imefanyizwa kwa vitu vinavyoelea, katikati kuna kitambaa chepesi sana, na chini kuna mnyororo wa chuma uliofunikwa kwa zinki ili kushikilia kitambaa hicho.

Kontena za kushughulikia takataka. Zaidi ya asilimia 70 ya takataka za ujenzi zilishughulikiwa na kupelekwa katika vituo rasmi vya kuziboresha ili zitumiwe tena.

Wafanyakazi wakipanda mimea karibu na mwingilio mkuu wa makao makuu ya Mashahidi. Bustani ilitia ndani miti, mimea, na nyasi za eneo hilo.

Wafanyakazi wakitayarisha mfumo wa kutumia nishati ya mvuke kutoka ardhini utakaozungusha maji mita 152 chini ya ardhi. Kiwango cha joto chini ya ardhi huwa cha wastani nyakati zote, ilhali juu ya ardhi hali ya joto hubadilika sana wakati wa kiangazi na wakati wa majira ya baridi kali. Mfumo wa nishati ya mvuke kutoka ardhini hudumisha kiwango kilekile cha joto mwaka mzima—kwa hiyo wakati wa majira ya baridi kali, mabomba hupashwa joto chini ya ardhi na hivyo maji yanayozunguka hulipasha joto jengo. Wakati wa kiangazi maji hayo yanayozunguka hutumiwa kuondoa joto katika jengo. Mfumo wa Mashahidi wa kutumia nishati ya mvuke kutoka ardhini unatazamiwa kupunguza nishati inayohitajika kupasha na kupoza kiwango cha joto katika majengo kwa asilimia 40.

Ndani ya Jengo la Ofisi na Huduma. Sehemu za ndani (k.m., rangi, kuta na dari) zinapatana na viwango vya Shirika la Majengo Yasiyoharibu Mazingira za kutumia bidhaa zisizotokeza uchafuzi mkubwa, na hivyo kuboresha afya ya watumiaji.