NEW YORK—Jumanne, Aprili 26, 2016, Mashahidi wa Yehova waliuza jengo lao la 124 Columbia Heights, Brooklyn, New York. Jengo hilo lenye ukubwa wa zaidi ya kilomita za mraba 14,121, liko kwenye upande wa kaskazini wa kijia cha Brooklyn Heights Promenade. Linajulikana sana kutokana na mnara wa mlinzi ulio juu yake. Tangazo la kuuzwa lilitolewa Desemba 2015, na baada ya wanunuzi mbalimbali kujitokeza, Mashahidi wa Yehova waliamua kumuuzia mteja mmoja ambaye hajawahi kununua majengo ya Mashahidi wa Yehova.

122-124 Columbia Heights kabla ya kurekebishwa na Mashahidi.

Mwanzoni jengo hilo la 124 Columbia Heights lilikuwa makazi ya Henry Ward Beecher, aliyepigania kukomesha biashara ya utumwa na aliyekuwa kasisi wa Kanisa la Plymouth, mwaka wa 1856 mpaka 1881. Gazeti la The New York Times liliripoti hivi kuhusu jengo hilo lenye historia muhimu: “Hii ndiyo nyumba ambayo inasemekana Rais Lincoln alimtembelea Bw. Beecher muda mfupi kabla ya kutia sahihi hati ya kuwaweka huru watumwa.” Mei 1909, Mashahidi walinunua jengo hilo pamoja na mengine yaliyokuwa jirani na kuyaunganisha kuwa jengo kubwa la ghorofa kumi.

Msemaji wa Mashahidi wa Yehova, Richard Devine, alisema hivi: “Tunaliona jengo la 124 Columbia Heights kuwa ni mojawapo ya majengo yenye historia ya pekee katika tengenezo letu. Tangu mwaka wa 1909, jengo hilo lilitumiwa kama makazi ya wafanyakazi wa kwenye makao yetu makuu ya ulimwenguni pote. Kuanzia mwaka 1929 mpaka 1957, kasoro miaka minne tu, jengo hilo la 124 Columbia Heights lilikuwa pia na kituo cha redio yetu ya WBBR, ambayo ilitangaza hotuba za Biblia na mambo yaliyohusiana na mafundisho ya Biblia.”

Studio kwa ajili ya kituo cha redio cha Mashahidi, WBBR, kwenye jengo ya 124 Columbia Heights miaka ya 1950.

Ingawa Mashahidi wamekuwepo Brooklyn Heights kwa zaidi ya miaka 100, makao makuu ya kwanza ya shirika la kisheria la Watch Tower Bible and Tract Society yalianzishwa miaka ya 1880 eneo la Allegheny (ambapo sasa ni sehemu ya Pittsburgh), Pennsylvania. David A. Semonian, msemaji wa Mashahidi kwenye makao makuu ya ulimwenguni pote anasema hivi: “Uamuzi uliofanywa mnamo 1909 wa kuhamia jiji la bandarini kama hili la Brooklyn ulikuwa wa maana sana katika kipindi hicho ambapo kazi ya elimu ya Biblia ilikuwa ikipanuka na kuongezeka kwa kasi sana.”

Kuuzwa kwa jengo la 124 Columbia Heights ni hatua ya karibuni zaidi ya Mashahidi kuhamisha makao yao makuu kwenye eneo la karibu ekari 50 la Warwick, New York ambapo hivi karibuni ujenzi wa ofisi hiyo utakamilika. Bw. Semonian anaongeza hivi: “Kuhamia kwenye majengo yetu hayo mapya yaliyoko nje ya jiji la New York ndilo jambo tunalohitaji hasa wakati huu. Tumekuwa Brooklyn kwa zaidi ya karne moja, na sasa kwa kuhamia Warwick tunafungua ukurasa mpya katika historia yetu.”

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

David A. Semonian, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1 718 560 5000