Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

NOVEMBA 1, 2016
MAREKANI

Mashahidi Wakarabati Bwawa Lililojengwa Miaka 60 Iliyopita Huko Warwick

Mashahidi Wakarabati Bwawa Lililojengwa Miaka 60 Iliyopita Huko Warwick

NEW YORK—Mnamo Agosti 2016 Mashahidi wa Yehova walikamilisha ujenzi wa makao yao makuu huko Warwick, New York. Ikiwa sehemu ya ujenzi huo, Mashahidi pia wamekamilisha kurekebisha Bwawa la Ziwa Blue, kazi waliyofanya kwa kushirikiana na kampuni ya SUEZ Water New York Inc.

Muda mfupi baada ya kununua uwanja huo mwaka wa 2009, Mashahidi walifanya mipango ili kukarabati Bwawa la Ziwa Blue lililokuwa limechakaa sana. Bwawa hilo (kwenye picha juu) liko kando ya Makao makuu mapya ya Mashahidi na bwawa hilo linahifadhi maji ya Ziwa Blue (pia linaitwa Ziwa Sterling Forest). Uchunguzi uliofanywa baadaye na Wizara ya Kuhifadhi Mazingira (DEC) ulithibitisha kwamba bwawa hilo lilikuwa linavuja maji na kwamba vali ya kufungua lango ili kuachilia maji yanapojaa ilikuwa imeharibika. Kwa kuwa kulikuwa na nyumba 195 katika eneo la Woodlands katika kata ndogo ya Tuxedo karibu na Ziwa Blue, DEC ilisema kwamba bwawa hilo ni hatari kwa usalama.

Makao makuu mapya ya Mashahidi wa Yehova (chini kushoto) kando ya Bwawa la Ziwa Blue (kulia katikati).

Jeffrey Hutchinson, aliyekuwa msimamizi wa Msitu wa Sterling.

Jeffrey Hutchinson, aliyekuwa msimamizi wa Msitu wa Kitaifa wa Sterling wakati huo alisema hivi: “Ilikuwa wazi kwamba bwawa hilo linavuja, na iwapo lingevunja kingo zake, madhara makubwa sana yangetokea. Nyumba zote zilizo katika kata ndogo ya Woodlands, au nyingi kati yake zingefagiliwa na maji hayo.”

Robert R. Werner, rais wa Shirika la Wamiliki wa Nyumba la Tuxedo, anasema: “Nina hakika kwamba ikiwa Mashahidi wa Yehova hawangekarabati bwawa hilo, mradi huo haungeshughulikiwa mpaka wakati ambapo bwawa hilo lingesababisha madhara. Ikiwa hilo lingetokea, tungepoteza mali na watu wengi wangepoteza uhai.”

Eneo la Woodlands katika kata ya Tuxedo (juu kushoto) liko karibu na makao makuu ya Mashahidi wa Yehova (chini kulia) na Bwawa la Ziwa Blue.

Bw. Hutchinson anaeleza hivi: “Mwaka wa 2011, Bwawa la Ziwa Echo, lililo umbali usiozidi kilomita 50 kutoka Ziwa Blue, lilivunja kingo zake na kusababisha uharibifu katika eneo la East Village lililoko Tuxedo, New York.” Wahandisi wa mji huo walikadiria kwamba kingo za Bwawa la Ziwa Echo zilipovunjika, zaidi ya lita milioni 350 za maji zilitiririka kwa kasi kuingia Mto Ramapo. Ziwa Echo lina ukubwa wa ekari 13. Kwa hiyo, ziwa hilo ni ndogo sana likilinganishwa na Ziwa Blue lililo na ukubwa wa ekari 115.

Bwawa la Ziwa Blue, lililotengenezwa mwaka wa 1956, liko kwenye upande wa mashariki wa ziwa hilo na mwanzoni lilikuwa na sehemu mbili: bwawa kuu la ardhini na mfereji wa saruji wa kupunguza maji. Vali ya usalama, ambayo hutumiwa kupunguza kiwango cha maji wakati wa dharura, iliwekwa kwenye kilindi cha Ziwa hilo.

Richard Devine, mwenyekiti wa Halmashauri ya Mradi wa Ujenzi wa Warwick ya Mashahidi anasema hivi: “Tunafurahi kwamba mradi wa kukarabati bwawa hilo ulifanikiwa, na bila shaka tunathamini msaada wa kampuni ya SUEZ Water. Wajenzi wetu walikarabati bwawa hilo, wakabadili vali ya zamani iliyokuwa imevunjika na kuweka mpya, wakaongeza mfereji wa ziada wa kupunguza maji, na kuukarabati mfereji wa saruji wa kupunguza maji ya bwawa ili uwe imara zaidi. Kukamilika kwa mradi huo kunahakikisha kwamba sasa bwawa hilo limefikia viwango vya usalama vilivyowekwa.”

Bw. Hutchinson anasema hivi kuhusu Mashahidi na kazi yao ya ujenzi: “Ninyi mnatimiza mambo mengi mazuri kwa ajili ya jamii yetu na mnasaidia mnapoweza. Kiwango chenu cha ujenzi ni cha hali ya juu na mnajali mazingira.”

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

David A. Semonian, Ofisi ya Habari za Umma, 1-718-560-5000

Wafanyakazi wa Watchtower wakiondoa vali iliyoharibika kutoka katika kilindi cha Ziwa Blue. Vali hiyo itasaidia kupunguza kiwango cha maji mafuriko yanapotokea.

Kifaa kipya cha kuzuia takataka kikiwekwa kwenye kilindi cha ziwa ili kuzuia takataka kubwa zisikwame ndani ya vali ya kutoa maji inapofunguliwa.

Wafanyakazi wa Watchtower wakipanua mfereji wa kupunguza maji ya bwawa. Maji yanayotoka yanapita juu ya mfereji huo wa kupunguza maji ya bwawa na kuingia kwenye kijito kilicho karibu.

Wafanyakazi wa Watchtower wakiinua pembe za mfereji wa saruji wa kupunguza maji ya bwawa kwa zaidi ya mita moja na pia wakirekebisha nyufa zilizokuwa katika mfereji huo.

Wakiondoa mchanga na kumimina aina fulani ya pekee ya kokoto iliyotengenezwa hasa kwa ajili ya kazi hii. Meta 19,000 hivi za mraba za kokoto zilihitajiwa ili kuimarisha bwawa hilo.

Mashine ya kusawazisha ikikamilisha kazi ya kusawazisha na kugandamiza kokoto.

Kikundi cha kutengeneza bustani kiliongeza udongo wa juu na kupanda nyasi za asili ambazo zingesaidia kufanya eneo hilo la bwawa lifanane na mazingira yake.