Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

MEI 13, 2015
MAREKANI

Mashahidi wa Yehova Wafungua Ofisi ya Utafsiri ya Lugha ya Ishara ya Marekani Florida

Mashahidi wa Yehova Wafungua Ofisi ya Utafsiri ya Lugha ya Ishara ya Marekani Florida

FORT LAUDERDALE, Florida—Novemba 14, 2014, Mashahidi wa Yehova walianza kuhamisha kikundi cha utafsiri cha Lugha ya Ishara ya Marekani (ASL) kutoka Watchtower Educational Center iliyopo Patterson, New York, kwenda Fort Lauderdale, Florida. Mashahidi wamekuwa wakitafsiri Biblia na machapisho yanayotegemea Biblia katika Lugha ya Ishara ya Marekani kwenye ofisi zao za Patterson tangu mwaka wa 1995. Katika miezi michache iliyopita, Mashahidi wamekuwa wakirekebisha majengo yao ya Fort Lauderdale na kutengeneza ofisi mpya na studio za kurekodi. Tangu Mei 2015, ofisi hiyo ilianza kazi rasmi.

Mashahidi hutokeza video katika lugha hiyo ya ishara na kuziweka mtandaoni katika tovuti ya jw.org na katika DVD. Pia zinatumika kikawaida kwenye mikutano ya kila juma katika makutaniko zaidi ya 500 ulimwenguni pote pamoja na makusanyiko madogo na ya eneo.

Jonathan Galvez, anayesimamia kikundi hicho cha utafsiri katika jimbo la Florida alisema hivi: “Lengo letu ni kuhakikisha kuwa video zetu zinaeleweka kwa urahisi na kwa idadi kubwa ya wanaotumia ASL, bila kujali nchi wanayotoka au kiwango chao cha elimu. ASL inatumika katika nchi 45 hivi na, kama ilivyo katika lugha za kawaida, viziwi pia wanatofautiana katika lugha ya ishara kulingana na eneo. Kwa kuwa sasa tumehamia katika jiji la Fort Lauderdale, watafsiri wetu wako katikati ya kikundi kikubwa cha watu kutoka mataifa mbalimbali wanaotumia lugha ya ASL.”

Mwaka wa 2014, Frank Bechter, mwenye shahada ya juu zaidi katika elimu ya binadamu inayohusu tamaduni na lugha, alihudhuria kusanyiko la eneo la Mashahidi wa Yehova katika ASL jijini Richmond, Virginia, ikiwa sehemu ya utafiti wake unaohusu lugha ya ishara na jamii ya viziwi. Dakt. Bechter alisema hivi: “Bidii yenu ya kutafsiri kwa kiwango cha hali ya juu katika ASL ilionekana wazi kabisa katika mkutano wa Richmond, hasa kupitia video zilizoandaliwa vizuri za tafsiri ya mistari ya Biblia. ASL iliyotumiwa humo ni nzuri sana. Ninathamini sana jitihada za Mashahidi za kutafsiri Biblia vizuri katika ASL, kwa kuwa ni hati muhimu sana katika jamii yetu na katika historia ya ulimwengu. Na ninaamini kwamba viziwi pia, kama tu watu wengine, wanapaswa kupata kwa urahisi hati muhimu ambazo zimeathiri historia ya ulimwengu.”

Vikundi vya utafsiri vya Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote vimetayarisha na kusambaza video nyingi katika lugha 80 hivi za ishara bila malipo. Mashahidi wa Yehova wametayarisha pia programu ya JW Library Lugha ya Ishara inayorahisisha upakuzi, upangaji, na uchezaji wa video zilizopo katika tovuti ya jw.org katika lugha ya ishara.

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

J. R. Brown, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1 718 560 5000