NEW YORK—Agosti 3, 2016, Mashahidi wa Yehova waliuza rasmi majengo yao ya 25/30 Columbia Heights, Brooklyn, New York, yaliyotumika kama makao makuu. Kuuzwa kwa majengo hayo, yaliyonunuliwa na makampuni ya Kushner na LIVWRK ni mojawapo ya hatua muhimu sana zilizochukuliwa na Mashahidi wa Yehova ili kuhamishia makao yao makuu kwenye jengo jipya na la kisasa lililopo Warwick, New York.

Majengo hayo yaliyo kwenye eneo lenye ukubwa wa mita 68,154 za mraba yako kati ya wilaya tatu za kihistoria, yaani, Brooklyn Heights, Fulton Ferry na Dumbo. Majengo matatu yaliyokuwa sehemu ya 25/30 Columbia Heights yalitiwa ndani pia ya uuzaji huo. Majengo hayo ni 50 Columbia Heights, 58 Columbia Heights na 55 Furman Street. Yote matatu yalijengwa kabla ya Daraja la Brooklyn lililopo karibu na majengo hayo.

50 Columbia Heights na 58 Columbia Heights

55 Furman Street

Awali majengo hayo ya 25/30 Columbia Heights yalimilikiwa na kampuni ya madawa iliyoitwa E.R Squibb & Sons ambayo sasa ni sehemu ya Bristol-Myers Squibb. Ishara ya saa na kipima joto iliyo juu ya jengo la 30 Columbia Heights imeonekana kwenye anga la Brooklyn kwa makumi ya miaka. Ishara hiyo ambayo awali iliandikwa “Squibb” ilibadilishwa na kuwa “Watchtower” baada ya majengo hayo kununuliwa na Mashahidi mwaka wa 1969. Richard Devine, msemaji wa Mashahidi anaeleza sababu ya kununuliwa kwa majengo hayo: “Tulihitaji nafasi kubwa zaidi ambayo ingetoshea kazi yetu iliyozidi kupanuka kwa haraka na pia tulitaka kuunganisha ofisi zetu ambazo wakati huo zilikuwa zimetawanyika katika majengo tofauti-tofauti kule Brooklyn.”

David A Semonian, msemaji wa Mashahidi wa Yehova katika makao makuu, anasema hivi: “25/30 Columbia Heights itaendelea kuwa sehemu ya urithi wetu wa pekee na pia sehemu ya historia ndefu ya Brooklyn.”

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

David A. Semonian, Ofisi ya Habari za Umma, 1-718-560-5000