Hamia kwenye habari

Mashahidi wa Yehova

Chagua lugha Kiswahili

FEBRUARI 14, 2014
KOREA KUSINI

Wakorea Waanza Kubadili Maoni Kuhusu Kukataa Utumishi wa Kijeshi kwa Sababu ya Dhamiri

Wakorea Waanza Kubadili Maoni Kuhusu Kukataa Utumishi wa Kijeshi kwa Sababu ya Dhamiri

SEOUL, Korea—Kulingana na kura ya maoni ya Gallup iliyofanywa hivi karibuni, Wakorea wengi sasa wanapendelea serikali ipange kuwe na utumishi wa badala kwa ajili ya wale ambao dhamiri inawazuia kujiunga na jeshi. Tangu Novemba 4-7, 2013, wanaume na wanawake Wakorea wapatao 1,211 walishiriki katika uchunguzi huo ambapo asilimia 68 kati yao walisema kwamba badala ya kuwafunga gerezani wale ambao dhamiri zinawazuia kujiunga na jeshi, inafaa kwa serikali kuwapa utumishi wa badala wa kiraia. Matokeo ya uchunguzi huo yanaonyesha kwamba watu nchini Korea wamebadili sana maoni yao kuhusiana na suala hilo, hasa ukizingatia kwamba katika mwaka wa 2008 ni asilimia 29 ya wale waliohusika katika uchunguzi kama huo waliopendelea utumishi wa badala wa kiraia.

Pia, inaonekana kwamba baadhi ya wanasheria nchini Korea wangependelea utatuzi mwingine wa suala hilo badala ya kuwafunga. Katika makala yake iliyokuwa na kichwa, “Tatizo Lililopo la Kuchagua Utumishi wa Kiraia Badala ya Utumishi wa Kijeshi,” Han In-seop, profesa wa Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Seoul, Kitengo cha Sheria, alisema hivi: “Hakuna hakimu anayeweza kupitisha hukumu na kusema kwamba watu wanaokataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri wanatenda kosa dhidi ya jamii au hawana maadili mazuri. Isitoshe hakuna wasiwasi kwamba watu hawa watatoroka na ndio maana hakuna agizo linalotolewa la kuwafunga chini ya ulinzi mkali. Kila mara hakimu anapotoa uamuzi wake kwamba wana hatia, hakimu huyo anabaki akijihisi vibaya na kusumbuka dhamiri.”

Suala hilo linalohusu haki ya kibinadamu liliangaziwa hivi karibuni katika sinema moja iliyotayarishwa na Halmashauri ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Korea. Kwenye sinema hiyo kuna kisehemu chenye kichwa “Ice River.” Kinaonyesha mmoja wa Mashahidi wa Yehova ambaye alikataa utumishi wa kijeshi. Mwelekezi wa sinema hiyo alisema kwamba aliamua kuitengeneza baada ya kugundua kwamba mamia ya Mashahidi wa Yehova hufungwa gerezani kila mwaka kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Kulingana na ripoti ya Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa iliyochapishwa mnamo Juni 2013, nchi ya Korea Kusini ndiyo yenye idadi kubwa zaidi ya Mashahidi waliofungwa gerezani kwa kukataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri, ikiwa na asilimia 93 ya Mashahidi wote duniani waliofungwa kwa sababu ya suala hilo.

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

J. R. Brown, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1 718 560 5000

Jamhuri ya Korea: Dae-il Hong, simu +82 31 690 0055