Belinda (jina la mwisho halijatajwa kwa sababu za usalama) akiwa na watoto watatu katika hospital huko Dundo, Angola. Mume wake aliuawa nchini Kongo, na hawajui mtoto na binti mmoja walipo. Belinda na binti yake mdogo kabisa, Ritinha, 2, walipata majeraha yaliyotokana na kufyatuliwa risasi, ilibidi mtoto akatwe mguu. Binti yake mwingine aliumia watu walipotumia panga kumshambulia.

KINSHASA, Kongo—Mashahidi wa Yehova wanatoa misaada na kuwategemeza kiroho waabudu wenzao walioathiriwa na vita vinavyoendelea katika eneo la Kasai katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Vurugu zinazosababishwa na makabila mbalimbali, wanamgambo wenye silaha, na vita vya wenyewe kwa wenyewe vimetokeza wakimbizi zaidi ya milioni 1.3, kutia ndani wakimbizi zaidi ya 30,000 waliokimbia eneo la Kasai na kuingia nchi jirani ya Angola. Wengi wa wakimbizi hao wameshambuliwa kikatili na wanapofika Angola wanahitaji matibabu kwa sababu ya kuchomwa moto au majeraha mabaya kwa kushambuliwa na panga na risasi. Ripoti za sasa zinaonyesha kwamba wakimbizi zaidi ya 870 nchini Angola ni Mashahidi wa Yehova na watoto wao wadogo, na kati yao, 10 hivi wana majeraha. Inasikitisha kwamba kufikia sasa Mashahidi wa Yehova 22 wameuawa.

Mwakilishi wa ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova nchini Angola akitembelea kikundi cha wazee kutoka Angola na Kongo, baadhi yao ni wakimbizi.

Robert Elongo, ambaye ni msemaji wa Mashahidi wa Yehova katika ofisi yao ya tawi jijini Kinshasa, anasema hivi: “Tunasikitika kwamba watu wengi sana wameuawa katika vita hivyo, hasa kwa sababu baadhi yao ni watoto wadogo. Baadhi yao wameshambuliwa kwa sababu tu walikuwa karibu na eneo la vita. Tunahangaikia sana usalama wa waabudu wenzetu na tumewahimiza wachukue tahadhari. Pamoja na ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova nchini Angola, tunafanya yote tuwezayo kuwaandalia msaada wa kimwili, kihisia, na hasa wa kiroho.”

Wakimibizi waliokimbilia msituni kwa sababu ya vita nchini Kongo, wakijenga nyumba.

Mashahidi wa Yehova nchini Angola na Kongo wameanzisha halmashauri za kutoa msaada ili zipange kazi kubwa na yenye kuendelea ya kutoa msaada. Wakimbizi wamepelekewa tani zaidi ya 31 za msaada, zinatia ndani matandiko, nguo, chakula, chandarua za mbu, na viatu, na vilevile kilo 525 za dawa. Daktari mmoja ambaye ni Shahidi wa Yehova ametembelea kambi za wakimbizi ili kuwashughulikia watu 135 wanaohitaji matibabu haraka.

Pia, wawakilishi wa ofisi za tawi nchini Angola na Kongo wamewatembelea wakimbizi kuwatia moyo kiroho, kwa mfano, wamekuwa na mikutano ya pekee yenye hotuba zilizokusudiwa kushughulikia mahitaji ya wakimbizi. Ingawa lugha kuu nchini Angola ni Kireno, mipango imefanywa ili wakimbizi wanufaike kwa kusikiliza ibada katika Tshiluba, moja kati ya lugha kuu nchini Kongo kama picha iliyo hapo juu inavyoonyesha.

Baraza Linaloongoza la Mashahidi wa Yehova linasimamia kazi ya kutoa misaada kutoka makao yao makuu huko Warwick, New York, wakitumia pesa zilizotolewa mchango kwa ajili ya kazi ya elimu ya Biblia ya ulimwenguni pote.

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

David A. Semonian, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1-845-524-3000

Angola: Todd Peckham, simu +244-923-166-760

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo: Robert Elongo, simu +243-81-555-1000