Asubuhi ya Oktoba 30, 2016, tetemeko la nchi lenye kipimo cha 6.6 lilitikisa eneo la katikati ya nchi ya Italia. Hilo ndilo tetemeko kubwa zaidi kuwahi kuikumba Italia tangu 1980. Ingawa watu 20 hivi waliumia, ripoti za awali zinaonyesha kwamba hakuna mtu aliyekufa.

Tetemeko hilo la nchi, ambalo kitovu chake kilikuwa karibu na mji wa Norcia, lilitokea baada tu ya matetemeko mawili ya nchi kutokea katika mji huo siku chache tu mapema. Jioni ya Oktoba 26, 2016, tetemeko la nchi lenye kipimo cha 5.5 lilitokea, likifuatwa na tetemeko la kipimo cha 6.1 saa mbili baadaye.

Matetemeko haya ya karibuni yalitokea karibu na sehemu ambayo mnamo Agosti 24 tetemeko lingine la nchi lilisababisha vifo vya watu wapatao 300.

Ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova nchini Italia inaripoti kwamba hakuna Shahidi aliyekufa au aliyeumia sana, lakini familia mbili hivi za Mashahidi zilipoteza nyumba zao katika matetemeko ya Oktoba 26, na kwamba nyumba za Mashahidi wengine wengi ziliharibiwa. Wazee katika maeneo hayo wanawasiliana na Mashahidi walio katika maeneo yaliyoathiriwa ili kujua mahitaji yao na ikiwa kuna uharibifu mwingine uliotokea, hasa kwa kuwa wengi bado wanakabiliana na madhara ya tetemeko la Agosti. Kama waathiriwa wengine, Mashahidi wengi hawana uhakika ikiwa nyumba zao zina misingi imara na kwa hiyo wamekuwa wakilala katika magari yao, katika mahema, au katika Majumba ya Ufalme, yaani, majumba ambayo Mashahidi hutumia kwa ajili ya ibada.

Baraza linaloongoza la Mashahidi wa Yehova linasimamia kazi ya kutoa misaada wakati wa msiba likiwa katika makao makuu yao, kwa kutumia pesa zilizochangwa kwa ajili ya kazi ya Mashahidi ya kuhubiri ya ulimwenguni pote. Kuna Mashahidi zaidi ya 251,000 nchini Italia.

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

David A. Semonian, Ofisi ya Habari za Umma, 1-718-560-5000

Italia: Christian Di Blasio, 39-06-872941