Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

MEI 6, 2015
GUATEMALA

Shule Nchini Guatemala Zaomba Machapisho ya Mashahidi ili Kukabili Tatizo la Jeuri

Shule Nchini Guatemala Zaomba Machapisho ya Mashahidi ili Kukabili Tatizo la Jeuri

MEXICO CITY—Shule tatu nchini Guatemala zimeomba machapisho ya Mashahidi wa Yehova kwa ajili ya masomo ya darasani. Mashahidi waliitikia ombi hilo kwa kutoa bila malipo jumla ya machapisho 3,500 katika lugha za Kihispania na Quiché. Quiché ni lugha ya Wamaya inayozungumzwa na Wahindi wenyeji wa Amerika, katika nyanda za juu zilizo magharibi mwa Guatemala.

Shule ya Msingi ya Paraje Xepec: Mwalimu akifundisha kwa kutumia Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia, kilichotolewa bila malipo na Mashahidi wa Yehova.

Shule hizo ziliwasiliana na Mashahidi wa Yehova kwa sababu ni miongoni mwa mashirika machache yanayochapisha vitabu katika lugha ya Quiché na wana machapisho kadhaa yanayozungumzia masuala yanayokabili vijana wa Guatemala. Katika hati rasmi kutoka katika Shule ya Msingi ya Paraje Xepec, Profesa Maria Cortez alieleza kuwa machapisho hayo yaliombwa “ili kuokoa viwango na kanuni muhimu za maadili katika jamii.”

Shule ya Msingi ya Elisa Molina de Sthall: Wanafunzi wakisoma Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia katika lugha ya Quiché.

Utafiti wa karibuni unaonyesha kuwa uhalifu na jeuri miongoni mwa vijana nchini Guatemala umeenea sana. Hivyo, nchini Guatemala mashirika kama Programu ya Kuzuia Jeuri (VPP) yameanzishwa kwa lengo la kuwaunganisha “wanafunzi, wazazi, walimu, wenye mamlaka, na jamii ili kuandaa maeneo salama yaliyo katika ujirani wa shule na kupanga mazoezi na mafunzo ya ufundi kwa vijana.” Kwa sababu ya miradi hiyo, Taasisi ya Taifa ya Elimu ya Msingi yenye Mafunzo ya Kilimo (INEBOA), Shule ya Msingi ya Elisa Molina de Sthall (EORM), na Shule ya Msingi ya Paraje Xepec, ziliagiza Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia katika lugha ya Quiché. INEBOA pia iliagiza vitabu vya Mashahidi kwa ajili ya vijana, Buku la 1 na la 2 la Maswali Ambayo Vijana Huuliza—Majibu Yafanyayo Kazi katika Kihispania. Shule hizo ziliwapatia pia wazazi nakala ili wawasaidie watoto wao kujiandaa kwa ajili ya masomo kwenye darasa la utamaduni. Pia, shule hiyo iliingiza katika mtaala wake video Mwana Mpotevu Arudi, iliyotayarishwa na Mashahidi wa Yehova.

Erick De Paz, msemaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Guatemala, alisema hivi: “Ingawa lengo letu hasa ni kushiriki ujumbe unaotegemea Biblia na watu wakiwa nyumbani, tunafurahi kwamba machapisho yetu yanatumiwa na walimu na wazazi kuwasaidia vijana.”

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

J. R. Brown, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1 718 560 5000

Guatemala: Juan Carlos Rodas, simu. +502 5967 6015

Mexico: Gamaliel Camarillo, simu +52 555 133 3048