Hamia kwenye habari

Mashahidi wa Yehova

Chagua lugha Kiswahili

DESEMBA 3, 2014
DENMARK

Mashahidi wa Yehova Wachochea Upasuaji Usiohusisha Damu Nchini Denmark

Mashahidi wa Yehova Wachochea Upasuaji Usiohusisha Damu Nchini Denmark

COPENHAGEN, Denmark—Vyombo mashuhuri vya habari nchini Denmark vimekuwa vikiripoti kwamba wahudumu wa afya wa jiji hilo wameanza kuwa na maoni mapya kuhusu matumizi ya damu. Jarida la Kristeligt Dagblad, liliripoti hivi, “imegunduliwa kwamba wagonjwa wengi hawahitaji kutiwa damu kama ilivyodhaniwa.” Ripoti hiyo iliendelea kusema kwamba “Mashahidi wa Yehova ndio wamesababisha kuanzishwa kwa upasuaji usiohusisha damu.” Kwa msingi wa imani yao ya kidini, Mashahidi wa Yehova zaidi ya 8,000,000 ulimwenguni pote, kutia ndani zaidi ya 14,000 nchini Denmark, hutafuta matibabu bora zaidi yasiyohusisha matumizi ya damu.

Hospitali nchini Denmark zina sifa ya kuwatia watu wengi sana damu kuliko nchi nyingine duniani. Hata hivyo, kwenye makala ya “Upasuaji Usiohusisha Damu Waongezeka,” kituo cha habari cha Politiken kilisema kuwa, “Mashahidi wa Yehova huwafanya madaktari watafute njia za badala” wanaposhughulikia matibabu ambayo wamezoea kutumia damu. Ili kuwahudumia wagonjwa walio Mashahidi wa Yehova, baadhi ya madaktari wametumia njia mbalimbali kama vile matumizi ya homoni (erythropoietin) na madini ya chuma na vitamini B kabla ya upasuaji, na matumizi ya dawa za kupunguza kuvuja kwa damu (antifibrinolytics) wakati wa upasuaji. Gazeti la The Copenhagen Post, linasema, “kila mwaka Mashahidi wa Yehova watano hadi kumi hufanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo katika Hospitali ya Chuo cha Aarhus iliyo Skejby” bila kuhusisha damu.

Rigshospitalet, hospitali inayoshughulikia magonjwa hususa na mojawapo ya taasisi kubwa zaidi nchini Denmark ya elimu ya sayansi ya tiba, ilianzisha mradi wa kudhibiti matumizi ya damu katika mwaka wa 2009 kwenye Mji Mkuu.

Wahudumu wa afya nchini Denmark wamekubali kuwa uthibitisho mwingi zaidi unaendelea kuonyesha kwamba kutiwa damu mishipani ni hatari. Hospitali ya Rigshospitalet, katika jiji la Copenhagen, ilianzisha mradi wa kudhibiti matumizi ya damu mwaka 2009. Gazeti Berlingske linaripoti kwamba mradi huo umesaidia kupunguza matumizi ya damu kwa kiasi kikubwa na “kupunguza madhara yanayosababishwa na damu na pia idadi ya vifo.” Hospitali nyingine nyingi katika Mji Mkuu zimejiunga na mradi huo, na hospitali katika miji mingine zinapanga kufanya hivyo.

Gazeti la Berlingske linaeleza kuhusu Dakt. Morten Bagge Hansen, mtafiti na mkuu katika benki ya damu ya Rigshospitalet, akisema kuwa hatua iliyopigwa nchini Denmark ya kupunguza matumizi ya damu ni “hatua kubwa inayowaletea wagonjwa faida kwelikweli.” Zaidi ya hayo, Redio Denmark na jarida la Kristeligt Dagblad zina mnukuu Dakt. Astrid Nørgaard, Mkurugenzi wa Afya katika hospitali ya Rigshospitalet, akisema kwamba “upasuaji usiohusisha damu usingekuwa umepiga hatua kubwa kadiri hii, bila Mashahidi wa Yehova.”

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

J. R. Brown, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1 718 560 5000

Denmark: Erik Jørgensen, simu +45 59 45 60 00