STRASBOURG, Ufaransa—Mnamo Septemba 25, 2012, Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu ilifikia mkataa kwamba serikali ya Austria ilikuwa na hatia ya kuwabagua Mashahidi wa Yehova nayo ikaamuru serikali hiyo ilipe kiasi cha karibu dola 16,000 za Marekani (euro 13,000) ili kulipia gharama na matumizi ya Mashahidi kuhusiana na mambo ya kisheria.

Katika mwaka wa 2002, serikali ya Austria ilikataa kuwapa kibali cha uraia wahudumu wawili wa Mashahidi wa Yehova kutoka Ufilipino ambao walitaka kufanya kazi ya uchungaji miongoni mwa Mashahidi wanaozungumza Kitagalog nchini Austria. Katika kisa kingine, serikali hiyo ilikuwa imewalazimisha Mashahidi walipe kodi kwa ajili ya michango ya kidini iliyokuwa imepokelewa katika mwaka wa 1999. Serikali ilichukua hatua hizo katika visa vyote viwili ili badala ya kuwatambua Mashahidi wa Yehova kama “shirika la kidini,” iwatambue tu kama “dini ya jamii.” Jambo hilo lilisababisha Mashahidi wanyimwe mapendeleo fulani ambayo dini nyingine zilizoimarika zilipata.

Hii ni mara ya sita kwa Mahakama hiyo kutoa uamuzi dhidi ya serikali ya Austria na kuwaunga mkono Mashahidi wa Yehova, na uamuzi huo unalingana na uamuzi uliokuwa umetolewa awali mwaka wa 2008. Katika uamuzi huo wa awali Mahakama ilikata kauli kwamba Mashahidi walipaswa kutambuliwa kama “shirika la kidini” ndani ya “kipindi kifupi sana cha wakati” kwa sababu Mashahidi wamekuwa “wakijulikana ulimwenguni kwa muda mrefu” na pia “wamekuwapo kwa muda mrefu” nchini Austria.

Mashahidi hao wanatumaini kwamba ushindi huo wa hivi karibuni katika Mahakama ya Ulaya utalinda haki za msingi na kuzuia ubaguzi wa kidini, si tu kwa faida ya waabudu wenzao bali pia kwa faida ya raia wote wanaoishi katika nchi ambazo ni wanachama wa Baraza la Ulaya.

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

J. R. Brown, Ofisi ya Habari za Umma, simu. +1 718 560 5000

Austria: Johann Zimmermann, simu. +43 1 804 53 45