Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

MEI 26, 2017
URUSI

Shahidi wa Yehova Kutoka Denmark Akamatwa na Kufungwa Gerezani Nchini Urusi Baada ya Polisi Kuvamia Mkutano wa Kikristo

Shahidi wa Yehova Kutoka Denmark Akamatwa na Kufungwa Gerezani Nchini Urusi Baada ya Polisi Kuvamia Mkutano wa Kikristo

NEW YORK—Baada ya uamuzi wa Mahakama Kuu ya Urusi iliyotolewa Aprili 20, 2017 dhidi ya Mashahidi wa Yehova, raia wa nchi ya Denmark alikamatwa na polisi pamoja na raia wa Urusi walipokuwa wakiabudu kwa amani Mei 25, 2017.

Dennis Christensen

Polisi 15 hivi wenye silaha kali na maofisa wa Usalama wa Taifa (FSB) walivamia ibada ya Mashahidi wa Yehova katika jiji la Oryol (linalojulikana pia kama Orel), kwenye picha juu. Polisi walikusanya vitambulisho vya watu wote waliohudhuria na kuchukua vifaa vyao vya kielektroni. FSB pia walimkamata Dennis Christensen, Shahidi wa Yehova ambaye ni raia wa Denmark. Muda mfupi baadaye, maofisa wa polisi walipekua nyumba nne za Mashahidi wa Yehova jijini humo.

Baada ya kukaa mahabusu usiku kucha, leo, Mahakama ya Wilaya ya Sovieti ya Oryol ilikubali ombi la FSB na kuagiza kwamba Bw. Christensen abaki gerezani akisubiri FSB ikamilishe uchunguzi wake kuhusiana na kesi hiyo. Bw. Christensen ndiye raia wa kwanza wa nchi nyingine kukamatwa tangu uamuzi wa Mahakama Kuu ya Urusi. Kuna uwezekano mkubwa kwamba Bw. Christensen atahukumiwa kifungo kirefu gerezani.

Huo ni uvamizi wa hivi karibuni zaidi kati ya matukio zaidi ya 40 dhidi ya Mashahidi wa Yehova yanayoendelezwa na wenye mamlaka na watu wengine baada ya Mahakama Kuu ya Urusi kuwatangaza Mashahidi kuwa wenye msimamo mkali na kufunga Kituo cha Usimamizi cha Mashahidi nchini Urusi pamoja na mashirika 395 ya kidini wanayotumia nchini kote.

Wavamizi waliteketekeza jumba linalotumiwa kwa ibada.

Saa chache tu baada ya Mahakama Kuu kutoa uamuzi wake Aprili 20, kikundi cha wanaume huko St. Petersburg kilivamia majengo makubwa zaidi ya Mashahidi wa Yehova nchini Urusi na hata kuwatisha waabudu. Wavamizi pia wamevamia majengo mengine ya ibada na hata nyumba za Mashahidi katika maeneo ya Kaliningrad, Moscow, Penza, Rostov, St. Petersburg, Sverdlovsk, Voronezh, na Krasnoyarsk. Katika kisa kimoja kilichotokea Mei 24, 2017, kwenye mji wa Zheshart katika Jamhuri ya Komi, jumba la ibada la Mashahidi wa Yehova liliharibiwa kwa kuteketezwa. Zaidi ya uvamizi wa polisi na raia wengine, Mashahidi mmoja-mmoja wameshambuliwa, kutishwa shuleni na kazini, au kufutwa kazi.

David A. Semonian, msemaji wa Mashahidi katika makao yao makuu, anasema hivi: “Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote wanahangaikia hata zaidi waabudu wenzetu nchini Urusi. Ni wazi kwamba matukio hayo mabaya yamesababishwa na uamuzi usio wa haki wa Mahakama Kuu ya Urusi. Tulikata rufaa uamuzi huo Mei 19, 2017. Hilo litawapa wenye mamlaka fursa nyingine ya kukomesha matendo hayo yasiyo ya haki dhidi ya Mashahidi wa Yehova. Pia, tumetuma malalamiko dhidi ya kufungwa isivyo haki kwa mwabudu mwenzetu, Dennis Christensen.”

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

David A. Semonian, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1-845-524-3000