ST. PETERSBURG, Urusi—Novemba 2014, Svetlana Nemchinova, Shahidi wa Yehova, aliokota barabarani bahasha yenye zaidi ya dola 6,800. Baada ya kumtafuta kwa muda mrefu mwenye pesa hizo, alifanikiwa kumpata na kuzirudisha. Tendo la unyofu la Bi. Nemchinova liliripotiwa katika televisheni, redio, na katika makala kadhaa zinazopatikana katika intaneti.

Bi. Nemchinova anafanya usafi wa barabara katika jiji la Vologda, kilometa 450 hivi kaskazini mashariki mwa jiji la Moscow. Akiwa kazini, aliona bahasha isiyo na maandishi yoyote. Alipotazama ndani, ilikuwa na kiasi kikubwa cha pesa. Ingawa Bi. Nemchinova na watoto wake watatu wanaishi katika nyumba ndogo, alieleza hivi: “Hata sikuwa na wazo la kutumia pesa hizo. Nilimfikiria aliyezipoteza ambaye kwa hakika alikuwa akihangaika sana.”

Ili kumpata mwenyewe, Bi. Nemchinova alibandika matangazo kwenye majengo yaliyokuwa karibu. Alipoona hakuna aliyejitokeza, Bi. Nemchinova alipeleka pesa hizo kwenye benki iliyo karibu, kwa kuwa ndani ya bahasha kulikuwa na risiti yenye jina la benki hiyo. Benki ilithibitisha kuwa pesa hizo zilikuwa za Pavel Smirnov. Baada ya benki hiyo kujaribu kwa mara kadhaa kuwasiliana na Bw. Smirnov, hatimaye ilifanikiwa kumjulisha kwamba Bi. Nemchinova alikuwa amezipata pesa zake.

Makala iliyochapishwa katika gazeti la Urusi liitwalo Premier lilieleza hivi: “Svetlana haoni jambo alilofanya kuwa la pekee. Yeye anamwamini Mungu na husoma Biblia kwa ukawaida.” Bi. Nemchinova alilieleza gazeti la Premier kwamba alitenda kulingana na ile iitwayo Kanuni Bora, inayopatikana katika Mathayo 7:12: “Kwa hiyo, mambo yote mnayotaka watu wawatendee ninyi, lazima mwatendee wao pia vivyo hivyo.”

Mchoraji Pavel Smirnov akiwa na Svetlana Nemchinova baada ya kumrudishia pesa zake.

Bw. Smirnov, ni mchoraji aliyebuni aina ya rangi ya pekee, na alikuwa akitunza pesa hizo ili anunue vifaa vya pekee kwa ajili kuendeleza utafiti wake wa rangi. Alisema hivi: “Siwezi kueleza ninavyomshukuru Svetlana. Tendo hilo limenisaidia kuanza kuwaamini tena watu. Sina budi kusema kuwa: ‘Mungu yupo!’”

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

J. R. Brown, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1 718 560 5000

Urusi: Yaroslav Sivulskiy, simu +7 812 702 2691