Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

Wajumbe kutoka kushoto kwenda kulia: Alberto Rovira (Hispania), Peter Hamadej (Slovakia), Andrejs Gevla (Latvia), Chong Ho (Korea), Yaroslav Sivulskiy (Urusi), Johann Zimmermann (Austria), Stefan Steiner (Uswisi), Vasiliy Kalin (Urusi), Tommi Kauko (Finland), Mark Sanderson (Marekani), Robert Delahaije (Uholanzi), Marc Hansen (Ubelgiji), Paul Gillies (Uingereza), Lars-Erik Eriksson (Sweden), Tommy Jensen (Denmark), Jørgen Pedersen (Norway), Manfred Steffensdorfer (Ujerumani), Teemu Konsti (Lithuania), Babis Andreopoulos (Ugiriki), Tambet Ernits (Estonia), Jean-Claude Pons (Ufaransa)

JULAI 21, 2017
URUSI

Wajumbe wa Kimataifa Wawaunga Mkono Ndugu Zao Warusi Wakati wa Rufaa ya Mahakama Kuu

Wajumbe wa Kimataifa Wawaunga Mkono Ndugu Zao Warusi Wakati wa Rufaa ya Mahakama Kuu

NEW YORK—Baraza Linaloongoza la Mashahidi wa Yehova lilipanga wajumbe wasafiri kutoka mabara matatu ili kuwaunga mkono ndugu na dada nchini Urusi.

Wajumbe hao walipofika, walikutana na ndugu na dada Warusi waliokuwa na furaha, na baadhi yao walikuwa wamesafiri kutoka maeneo ya mbali sana kama Siberia kwenda Moscow. Wajumbe hao waliwahakikishia ndugu na dada Warusi kwamba wanawahangaikia sana na kwamba ndugu ulimwenguni pote wanatoa sala kwa niaba yao. Mjumbe mmoja alisema hivi: “Niliguswa sana na mtazamo wa ujasiri wa ndugu zangu Warusi, hasa kwa sababu kulikuwa na uwezekano mdogo sana wa kubatilishwa kwa uamuzi huo usio wa haki wa kupiga marufuku utendaji wao.”

Licha ya uamuzi usiofaa wa mahakimu watatu, mahakama ilijawa na watu waliopendana kikweli na wenye umoja. Walihuzunika sana kusikia jina la Yehova likishutumiwa hadharani na walitambua kwamba Mashahidi wa Yehova nchini Urusi wangekabili kipindi kigumu. Hata hivyo, kwa kuwa ndugu na dada walijiendesha kwa upendo na heshima mahakamani, huo ulikuwa uthibitisho tosha kwamba hawakuwa na “msimamo mkali” kama mahakimu wa rufaa walivyohukumu.

Mark Sanderson, mshiriki wa Baraza Linaloongoza alikuwa mmoja wa wajumbe hao. Aliwatia moyo akina ndugu “wawe wenye nguvu na jasiri” baada ya hukumu hiyo. Wajumbe hao walipoondoka mahakamani, Mashahidi wenyeji waliwakumbatia na kueleza kwamba walithamini kutegemezwa katika tukio hilo muhimu.

Wajumbe hao pia walitembelea balozi 21 jijini Moscow ili kutoa habari sahihi kuhusu matokeo mabaya ya shambulizi la Urusi dhidi ya Mashahidi wa Yehova. Habari hizo zilitia ndani kuteketezwa kwa nyumba za Mashahidi, kupoteza kazi, watoto kushambuliwa shuleni, na mashtaka ya uhalifu dhidi ya wazee kadhaa kwa sababu ya kupanga mikutano ya Kikristo, kutia ndani Ndugu Dennis Christensen, ambaye bado amefungwa kabla ya kusikilizwa kwa kesi yake. Mabalozi kadhaa walihuzunishwa sana na video ya dakika mbili iliyoonyesha matukio hayo kwa ufupi. Swali la kawaida ambalo maofisa waliuliza ni, ‘Kwa nini Mashahidi wa Yehova wananyanyaswa?’ Ndugu zetu waliwajibu kwa kutoa ushahidi wa nguvu kwa kueleza kwamba washiriki wa tengenezo letu hawaungi mkono upande wowote katika siasa na kwamba kazi yetu ya kuhubiri imebadili na kuboresha maisha ya Warusi wengi. Balozi mmoja alisema hivi: “Kanisa Othodoksi halitaki mvue samaki katika maji yao.” Balozi zaidi ya kumi zilituma wawakilishi mahakamani, nao walibaki hapo kwa kipindi chote cha saa nane.

Wajumbe hao wa kimataifa waliondoka nchini Urusi imani yao ikiwa imeimarishwa, wakiwa wametiwa moyo na azimio la ndugu Warusi kuendelea kuwa washikamanifu, na walifurahia nafasi waliyopata ya kuwatolea maofisa ushahidi.

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

David A. Semonian, Ofisi ya Habari za Umma, +1-845-524-3000