NOVEMBA 19, 2025
VENEZUELA
Miaka 100 ya Kuhubiri Habari Njema Nchini Venezuela
Mwaka wa 2025 unatimiza miaka 100 tangu habari njema ilipoanza kuhubiriwa nchini Venezuela. Venezuela ni nchi maridadi yenye mimea na wanyama wa aina mbalimbali. Isitoshe, kuna lugha nyingi zinazozungumzwa nchini humo. Kazi ya Ufalme ilianza nchini Venezuela mwaka wa 1925. Mwaka huo, ndugu mmoja kutoka Trinidad alipewa mgawo wa kuhubiri katika miji mikubwa nchini humo. Baadaye mwaka huo, Gazeti la Mnara wa Mlinzi liliripoti kwamba alisambaza nakala 35,000 za machapisho yanayotegemea Biblia kotekote nchini. Kazi hiyo ilikuwa msingi wa ukuzi wa kiroho.
Miaka kumi hivi baadaye, Dada Kate Goas na binti yake, Marion, kutoka Texas, Marekani, waliiandikia makao makuu na kuomba kutumikia katika nchi inayozungumza Kihispania. Walisafiri kwa meli na mwaka wa 1936, waliwasili Caracas, mji mkuu wa Venezuela. Walihubiri kwa bidii kwa miaka kumi. Na Aprili 10, 1946, wenyeji wa kwanza wa nchi hiyo walibatizwa. Pindi hiyo ilikuwa ya pekee sana kwa sababu walibatizwa kwenye kidimbwi cha asili chini ya maporomoko ya maji wakati wa ziara ya Ndugu Nathan Knorr na Ndugu Frederick Franz kutoka makao makuu.
Miezi miwili baadaye, yaani Juni 1946, Ndugu Donald Baxter na Ndugu Walter Wan waliwasili nchini Venezuela baada ya kuhitimu katika darasa la tano la Shule ya Gileadi. Kufikia Septemba, ofisi ya kwanza ya tawi nchini humo ilifunguliwa. Wakati huo, kulikuwa na wahubiri 19 tu nchini Venezuela. Tangu 1946, ambapo Ndugu Baxter na Ndugu Wan waliwasili nchini Venezuela, wamishonari wengine 140 wametumikia kwa bidii nchini humo na kuwasaidia watu wengi kujifunza kweli za Biblia. Leo kuna ndugu na dada 139,000 nchini Venezuela ambao wanahubiri habari njema katika Kihispania, Lugha ya Ishara ya Venezuela, na katika lugha nyingine 13 za asili kutia ndani Kipemon, Kipiaroa, Kiwarao, Kiwayuunaiki, na Kiyukpa.
Ofisi ya tawi ya sasa iliyo La Victoria, Venezuela
Tunashangilia kuona jinsi Yehova amewabariki ndugu na dada zetu nchini Venezuela katika miaka hiyo 100 iliyopita. Ni wazi Yehova yuko pamoja na wote wanaotangaza “habari njema ya Ufalme.”—Matendo 8:12.

