Kiswahili
Walinzi wa Gereza Wawapiga Ndugu Watano Huko Orenburg, Urusi
https://cms-imgp.jw-cdn.org/img/p/702020155/univ/art/702020155_univ_sqr_xl.jpg

Kushoto kwenda kulia: Aleksey Budenchuk, Konstantin Bazhenov, Feliks Makhammadiyev, Aleksey Miretskiy, Roman Gridasov, na Gennadiy German, kabla ya kukamatwa

FEBRUARI 17, 2020
URUSI

Walinzi wa Gereza Wawapiga Ndugu Watano Huko Orenburg, Urusi

Walinzi wa Gereza Wawapiga Ndugu Watano Huko Orenburg, Urusi

Februari 6, 2020, walinzi wa gereza la Penal Colony No. 1 huko Orenburg, Urusi, waliwapiga sana ndugu zetu watano kwa marungu. Ndugu hao ni Aleksey Budenchuk, Gennadiy German, Roman Gridasov, Feliks Makhammadiyev, na Aleksey Miretskiy. Ilibidi Ndugu Makhammadiyev apelekwe hospitali kwa sababu walinzi hao walimvunja ubavu, wakatoboa pafu lake, na kuharibu figo yake. Baada ya kuwapiga Ndugu Budenchuk, German, Gridasov, na Miretskiy, waliwapeleka kwenye chumba cha upweke kwa madai yasiyo na msingi na ya uwongo. Moja kati ya madai hayo ni kuvuta sigara—zoea ambalo halikubaliwi na Mashahidi wa Yehova.

Kama ilivyoripotiwa awali, Septemba 19, 2019, Hakimu Dmitry Larin wa Mahakama ya Wilaya ya Leninsky huko Saratov aliwahukumu ndugu hao watano pamoja na ndugu mwingine wa sita, Konstantin Bazhenov. Walihukumiwa vifungo vya kuanzia miaka miwili hadi miaka mitatu na nusu gerezani. Desemba 20, 2019, Mahakama ya Mkoa ya Saratov ilikataa rufaa yao. Majuma machache baadaye, ndugu wote sita walihamishiwa gerezani. Ndugu Bazhenov alipelekwa katika gereza la Penal Colony No. 3 katika mkoa wa Ulyanovsk Region kwa hiyo hakuwa na wale ndugu wengine watano walioteswa katika gereza la Penal Colony No. 1.

Februari 6, 2020, baada tu ya ndugu hao watano kufika katika gereza la Penal Colony No. 1, walipigwa. Hawakufanyiwa uchunguzi na daktari hadi siku iliyofuata ilipojulikana kwamba Ndugu  Makhammadiyev alikuwa na homa kali, na mkojo wake ulichanganyika na damu. Uongozi wa gereza uliita gari la wagonjwa baada ya kumlazimisha Ndugu Makhammadiyev atie sahihi karatasi iliyoonyesha kwamba aliumia kwa sababu “aliteleza na kuanguka bafuni.” Ndugu Makhammadiyev alilazwa na kufanyiwa upasuaji. Upasuaji huo ulihusisha kuingizwa mrija ndani ya pafu lake ili kuondoa maji yaliyokuwa yamejikusanya. Pia vipimo vilionyesha kwamba Ndugu Makhammadiyev alikaa kwa muda mrefu bila kula, kwa sababu ana ugonjwa unaomlazimu kula aina fulani ya chakula tu na uongozi wa gereza ulimnyang’anya chakula anachopaswa kula.

Tunawasikitikia sana ndugu zetu nchini Urusi wanapoendelea kuvumilia vitendo visivyo vya haki na vya kikatili. Hata hivyo, tunaamini kwamba Yehova ataendelea kuwategemeza wanapoendelea kuvumilia kwa uaminifu.—Wafilipi 1:27, 28.