Kiswahili
Urusi Yajiondoa Katika Mahakama ya Ulaya
https://cms-imgp.jw-cdn.org/img/p/702022224/univ/art/702022224_univ_sqr_xl.jpg

Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu iliyo jijini Strasbourg, nchini Ufaransa

JUNI 29, 2022
URUSI

Urusi Yajiondoa Katika Mahakama ya Ulaya

Urusi Yajiondoa Katika Mahakama ya Ulaya

Juni 11, 2022, Rais Vladimir Putin alitia sahihi miswada miwili kuwa sheria ili Urusi ijiondoe chini ya mamlaka ya Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu bila idhini ya mahakama hiyo kuanzia Machi 15, 2022. Hivyo, hukumu zote zilizotolewa na mahakama hiyo dhidi ya Urusi kuanzia Machi 15, 2022, na kuendelea hazitatekelezwa na Urusi. Hiyo inatia ndani hukumu iliyotolewa Juni 7 na mahakama hiyo, iliyosema kwamba kupigwa marufuku kwa Mashahidi wa Yehova ni kinyume na sheria na kuitaka Urusi isitishe kesi zote za uhalifu dhidi ya Mashahidi wa Yehova, iwaachilie huru Mashahidi ambao bado wapo gerezani, na irudishe maeneo iliyotaifisha ya Mashahidi wa Yehova au ilipe fidia ya euro milioni 59 (dola milioni 63 za Marekani).

Halmashauri ya Mawaziri wa Baraza la Ulaya husimamia utekelezaji wa maamuzi ya Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu katika nchi zilizo katika baraza hilo. Urusi imekuwa sehemu ya Baraza hilo tangu mwaka wa 1996.

Machi 15, 2022 Urusi ilitoa taarifa kuhusu uamuzi wake wa kujiondoa kwenye Baraza hilo. Siku iliyofuata, Baraza hilo liliiondoa Urusi. Kupatana na hilo serikali ya Urusi ilijulishwa kwamba kulingana na masharti ya mkataba ambao ilitia sahihi baada ya kujiunga na Baraza la Ulaya, Urusi itaendelea kuwa chini ya mamlaka ya Baraza la Ulaya hadi Septemba 16, 2022.

Juni 7, 2022, Urusi iliamua kujiondoa kutoka kwenye Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu bila kutimiza majukumu yake kwa mahakama hiyo kwa kupitisha miswada hiyo miwili iliyotajwa hapo juu. Hiyo ilikuwa ni siku ambayo Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu ilitoa hukumu iliyowaunga mkono Mashahidi wa Yehova nchini Urusi.

Hukumu ya Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu itatumiwa na mahakama za chini za nchi 46 zilizo chini ya Baraza hilo katika kesi zinazowahusu Mashahidi wa Yehova. Na hata jambo muhimu zaidi ni kwamba mahakama hiyo imeweka wazi kwamba Urusi haina msingi wowote wa kisheria wa kuwashtaki Mashahidi wa Yehova. Ulimwenguni pote, uamuzi huu umetoa ushahidi mkubwa kumhusu Yehova na kuliletea utukufu jina lake. Sifa zote zinamwendea Yehova!—Zab. 83:18