DESEMBA 17, 2019
URUSI
Mahakama ya Urusi Yamhukumu Ndugu Alushkin Miaka Sita Gerezani, na Wengine Watano Wanasubiri Kifungo
Ijumaa asubuhi, Desemba 13, 2019, Mahakama ya Wilaya ya Leninsky huko Penza ilimhukumu Vladimir Alushkin miaka sita gerezani. Alifungwa pingu papo hapo na kuwekwa chini ya ulinzi. Na wengine watano kutia ndani Tatyana, mke wa Vladimir, ni washtakiwa katika kesi hiyohiyo. Mahakama iliamua kwamba wote watano (ndugu watano na dada wawili) watasubiri kifungo cha miaka miwili gerezani. Ndugu na dada wote sita wanaoishi Penza watakata rufaa ya uamuzi huo.
Kama ilivyotangazwa awali, Vladimir Alushkin alikamatwa Julai 15, 2018, baada ya nyumba yake kuvamiwa na polisi 12 hivi wenye bunduki na waliofunika nyuso zao. Polisi hao walifanya msako katika nyumba hiyo kwa saa nne hivi, wakachukua simu za mkononi, vifaa vya kielektroni, Biblia, na machapisho yanayotegemea Biblia. Maofisa hao walifanya msako katika nyumba nyingine tano za Mashahidi wa Yehova na kuwapeleka ndugu na dada 40 hivi kwenye vituo vya polisi ili wakahojiwe.
Wenye mamlaka katika eneo hilo walimweka Ndugu Alushkin kizuizini kwa siku mbili kabla ya Mahakama ya Wilaya ya Pervomayskiy huko Penza kuagiza kwamba awekwe mahabusu kwa miezi miwili. Baada ya hapo mahakama hiyo ya wilaya iliongeza mara mbili muda wa Vladmir Alushkin kukaa kizuizini. Baada ya kukaa karibu miezi sita kuzuizini, alihamishwa na kupelekwa kwenye kifungo cha nyumbani, kilichoendelea mpaka siku aliyohukumiwa, Desemba 13.
Ndugu wengine watatu kati ya wale watano walioshtakiwa kwa kosa la uhalifu katika kesi hiyohiyo ni Ndugu Vladimir Kulyasov, Andrey Magliv, na Denis Timoshin. Wamekuwa katika kifungo cha nyumbani kipindi chote cha uchunguzi na kesi ilipokuwa ikiendelea. Na wale dada wengine wawili ni Dada Tatyana Alushkina na Galiya Olkhova, ambao walipewa dhamana tangu Februari 2019 ambayo iliwanyima uhuru wa kusafiri na kuwasiliana na wengine.
Agosti 2019, Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Vifungo Visivyo vya Haki (WGAD) ilichapisha ripoti yenye kurasa 12 ambayo ilishutumu Urusi kwa kumkamata na kumweka kizuizini Ndugu Alushkin. Kulingana na WGAD, Ndugu Alushkin “hakupaswa kukamatwa na kuwekwa kizuizini, na Bw. Alushkin hapaswi kufunguliwa mashtaka.” WGAD ilisisitiza kwamba “suluhisho ni kumwachilia huru Bw. Alushkin haraka iwezekanavyo.” Mawakili waliowatetea ndugu na dada hao wa Penza, walitumia hoja zinazotegemea ripoti ya WGAD. Hata hivyo, katika hukumu iliyosomwa Desemba 13, hakimu alisema kwamba mahakama imefuata hukumu ya 2017 ya Mahakama Kuu ya Urusi—ambayo ilipiga marufuku ibada ya Mashahidi wa Yehova—badala ya ripoti ya WGAD.
Kufikia sasa serikali ya Urusi imewafunga ndugu na dada 18 mwaka huu, na 9 kati ya ndugu hao wamehukumiwa vifungo vyenye urefu mbalimbali. Zaidi ya ndugu na dada 40 wamekuwa kizuizini na 19 wako katika kifungo cha nyumbani. Karibu ndugu na dada 300 nchini Urusi wanakabili mashtaka ya uhalifu kwa sababu ya imani yao.
Ingawa tunasikitika kusikia kuhusu minyanyaso ambayo ndugu na dada zetu wanakabili, hatushangazwi na majaribu hayo. Ni mambo ambayo yalitabiriwa, na Yehova aliahidi kwamba atawasaidia. Tunasali ‘roho ya utukufu, yaani roho ya Mungu, itulie juu yao.’—1 Petro 4:12-14.

