Kiswahili
Vitabu vya Biblia Vyatolewa Katika Lugha Mbili za Ishara Machi 2025
https://cms-imgp.jw-cdn.org/img/p/702025043/univ/art/702025043_univ_sqr_xl.jpg

MACHI 21, 2025
HABARI ZA ULIMWENGUNI POTE

Vitabu vya Biblia Vyatolewa Katika Lugha Mbili za Ishara Machi 2025

Vitabu vya Biblia Vyatolewa Katika Lugha Mbili za Ishara Machi 2025

Lugha ya Ishara ya Korea

Machi 8, 2025, Ndugu Stephen Lett, mshiriki wa Baraza Linaloongoza, alitangaza kutolewa kwa Biblia Takatifu—Tafsiri ya Ulimwengu Mpya ikiwa nzima katika Lugha ya Ishara ya Korea. Tangazo hilo lilitolewa katika mkutano wa pekee uliofanywa Goyang, Korea Kusini. Watu 7,226 walihudhuria programu hiyo uso kwa uso, na wengine 64,960 waliunganishwa kupitia video mtandaoni. Mara tu baada ya tangazo hilo, Biblia hiyo iliwekwa kwenye tovuti ya jw.org na kwenye programu za JW Library na JW Library Sign Language ili ipatikane kwa ajili ya kupakuliwa.

Hii ndiyo tafsiri ya kwanza kabisa ya Biblia nzima kuwahi kutolewa katika Lugha ya Ishara ya Korea. Leo, kuna watu 100,000 hivi wanaotumia Lugha ya Ishara ya Korea, kutia ndani zaidi ya ndugu na dada 1,700 wanaotumikia katika makutaniko 39 na vikundi 2 vya lugha ya ishara nchini Korea Kusini.

Lugha ya Ishara ya Ghana

Machi 16, 2025, Ndugu Joel Grim, mshiriki wa Halmashauri ya Tawi ya Ghana, alitangaza kutolewa kwa kitabu cha Biblia cha Mathayo katika Lugha ya Ishara ya Ghana katika mkutano wa pekee uliofanywa jijini Kumasi. Jumla ya watu 1,554 walihudhuria programu hiyo uso kwa uso na wengine 424 waliunganishwa kupitia video mtandaoni. Mara tu baada ya tangazo hilo, kitabu hicho kiliwekwa kwenye tovuti ya jw.org na kwenye programu za JW Library na JW Library Sign Language ili kipatikane kwa ajili ya kupakuliwa.

Hiki ni kitabu cha kwanza cha Biblia kuwahi kutafsiriwa katika Lugha ya Ishara ya Ghana. Inakadiriwa kuwa watu 211,000 hivi hutumia lugha hiyo leo. Kwa sasa, kuna zaidi ya ndugu na dada 1,250 wanaotumikia katika makutaniko 32 na vikundi 35 vya Lugha ya Ishara ya Ghana kotekote nchini humo.