Kiswahili
Mahakama ya Ulaya Yatoa Uamuzi Wake wa Mwisho Katika Suala la Uhuru wa Kuabudu Nchini Urusi na Lithuania
https://cms-imgp.jw-cdn.org/img/p/702022276/univ/art/702022276_univ_sqr_xl.jpg

Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu iliyo Strasbourg, Ufaransa

SEPTEMBA 29, 2022
HABARI ZA ULIMWENGUNI POTE

Mahakama ya Ulaya Yatoa Uamuzi Wake wa Mwisho Katika Suala la Uhuru wa Kuabudu Nchini Urusi na Lithuania

Mahakama ya Ulaya Yatoa Uamuzi Wake wa Mwisho Katika Suala la Uhuru wa Kuabudu Nchini Urusi na Lithuania

Septemba 7, 2022, Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) ilitoa uamuzi wake wa mwisho katika hukumu mbili muhimu sana zinazowahusu Mashahidi wa Yehova. Juni 7, 2022, ECHR ilitangaza kwamba serikali ya Urusi ilivunja sheria ilipowapiga marufuku Mashahidi wa Yehova nchini humo mwaka wa 2017. Siku hiyo hiyo, ECHR ilitoa uamuzi mwingine dhidi ya serikali ya Lithuania kwa sababu ya kutenda kinyume na Mkataba wa Ulaya wa Haki za Kibinadamu katika kesi inayomhusu Ndugu Stanislav Teliatnikov, ambaye alikataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri.

Nchi zote mbili, yaani, Urusi na Lithuania hazikukata rufaa kwenye Baraza Kuu la ECHR ili uamuzi huo uliotolewa Juni 7, upitiwe upya. Hivyo basi, nchi hizo mbili zimeamuriwa kutii masharti ya uamuzi huo, kutia ndani sharti la kuwalipa fidia watu wanaohusika kwenye kesi hizo.

Juni 11, 2022, nchi ya Urusi ilijaribu kukimbia wajibu huo kwa kujiondoa kwenye ECHR. Hata hivyo, ECHR bado ina mamlaka ya kufanya uamuzi katika kesi zilizofunguliwa dhidi ya Urusi kabla ya Septemba 16, 2022. Urusi inakabili mashtaka ya kukiuka makubaliano yaliyo katika Mkataba wa Ulaya wa Haki za Kibinadamu.

Tunasali kwamba nchi hizo zitekeleze maamuzi haya ya mwisho yaliyofanywa na ECHR na pia ziheshimu haki ya uhuru wa kuabudu ili Wakristo wanaopenda amani waendelee “kuishi kwa amani na utulivu na ujitoaji-kimungu kamili.”​—1 Timotheo 2:1, 2.