Kiswahili
Ndugu Watatu Wafungwa Gerezani Nchini Ukrainia Februari na Machi 2025 kwa Kukataa Kujiunga na Jeshi kwa Sababu ya Dhamiri
https://cms-imgp.jw-cdn.org/img/p/702025077/univ/art/702025077_univ_sqr_xl.jpg

APRILI 23, 2025
UKRAINIA

Ndugu sita wafungwa kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri Februari na Machi 2025 nchini Ukrainia

Ndugu Watatu Wafungwa Gerezani Nchini Ukrainia Februari na Machi 2025 kwa Kukataa Kujiunga na Jeshi kwa Sababu ya Dhamiri

Ndugu Wengine Watatu Wawekwa Mahabusu

Ndugu Watatu Wafungwa Gerezani Nchini Ukrainia Februari na Machi 2025 kwa Kukataa Kujiunga na Jeshi kwa Sababu ya Dhamiri

Kama ilivyoripotiwa kwenye jw.org, Januari 2025, Ndugu Vitalii Kryushenko alikuwa Shahidi wa kwanza kufungwa gerezani nchini Ukrainia kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri tangu vita vilipoanza. Kisha, serikali ya Ukrainia iliwafunga ndugu wengine sita waliokataa kutumikia jeshini kwa sababu ya dhamiri.

Andrii Khomenko na Iryna, mke wake

Februari 3, 2025, Ndugu Andrii Khomenko, mwenye umri wa miaka 50, alianza kutumikia kifungo cha miaka mitatu gerezani. Yeye na Iryna, mke wake, wana vijana wawili wa kiume. Muda mfupi kabla ya kupelekwa gerezani, Andrii alisema hivi: “Nina uhakika kwamba hata katika hali mbaya zaidi, sikuzote Yehova atakuwa tayari kunitegemeza na kunipa amani ya moyoni.”

Serhii Ivanushchenko

Juma moja hivi baadaye, yaani, Februari 11, 2025, Ndugu Serhii Ivanushchenko, mwenye umri wa miaka 48, alianza pia kutumikia kifungo cha gereza cha miaka mitatu. Serhii alibatizwa Novemba 2023 na baada ya miezi michache tu akaitwa ajiunge na jeshi. Hata hivyo, kwa kuwa Serhii anasadiki kwamba watumishi wa Mungu “hawatajifunza vita tena kamwe,” alienda mbele ya kamati inayowaandikisha watu jeshini, na kwa heshima akakataa kujiunga na jeshi.​—Isaya 2:4.

Serhii Nechaiuk

Kisha, Machi 5, 2025, maofisa wa serikali walimfunga gerezani Ndugu Serhii Nechaiuk, mwenye umri wa miaka 35. Nechaiuk amefunga ndoa na ana watoto wawili. Alipokuwa akijiandaa kuanza kifungo chake cha gereza cha miaka mitatu, alisema hivi: “Ndugu na dada zangu wanasali kwa ajili yangu. Sala zao za kutoka moyoni zinanithibitishia kwamba siko peke yangu. Yehova yuko nami.”

Isitoshe, kati ya Januari na Machi 2025, wanajeshi waliwasafirisha kwa lazima Ndugu Mykhailo Adamovych (mwenye umri wa miaka 40), Ndugu Yaroslav Bodnarchuk (28), na Ndugu Oleksandr Radashko (35) na kuwapeleka kwenye kituo cha wanajeshi. Kulingana na sheria ya nchi ya Ukrainia, ndugu hao wanaonwa kuwa wameanza utumishi wa kijeshi kwa sababu wamefikishwa katika kituo hicho cha wanajeshi. Hata hivyo, ndugu hao walipoamrishwa wavae sare za jeshi na wachukue silaha, walikataa kwa sababu ya dhamiri. Walishtakiwa kwa kutotii amri za jeshi na wakawekwa kizuizini. Kwa sasa, Mykhailo na Oleksandr bado wanazuiliwa wakisubiri kesi yao isikilizwe; Yaroslav aliachiliwa kwa dhamana. Ikiwa watapatikana na hatia, wanaweza kuhukumiwa kifungo cha kuanzia miaka mitano hadi kumi hivi gerezani.

Kushoto kwenda kulia: Mykhailo Adamovych, Yaroslav Bodnarchuk, na Oleksandr Radashko

Matendo hayo ya wenye mamlaka yanakiuka sheria za kimataifa na za Ukrainia. Kwa mfano, Kifungu cha 18 cha Azimio la Watu Wote la Haki za Kibinadamu na Kifungu cha 9 cha Mkataba wa Ulaya Kuhusu Haki za Kibinadamu vinasema kwamba mtu ana haki ya kutumikia utumishi wa badala wa kiraia ikiwa hatatumikia jeshini. Hapo awali, serikali ya Ukrainia ilikuwa imekubali kufuata sheria hizo za kimataifa. Pia, Katiba ya Ukrainia inasema kwamba mtu ana haki ya kutumikia utumishi wa badala wa kiraia usio wa kijeshi badala ya utumishi wa kijeshi.

Tukiwa undugu wa ulimwenguni pote, tunasali kwamba Yehova aendelee kuwafariji na kuwalinda ndugu hao waaminifu na wote wanaoendelea kujitahidi kuwa washikamanifu kwa Yehova.​—Zaburi 34:7.