DESEMBA 9, 2019
TURKMENISTAN
Mahakama ya Turkmen Imemhukumu Ndugu Dovletov Miaka Mitatu Gerezani kwa Kukataa Kujiunga na Jeshi
Novemba 12, 2019, mahakama ya Turkmenistan imemhukumu Ndugu Serdar Dovletov mwenye umri wa miaka 26 kifungo cha miaka mitatu gerezani. Ndugu Dovletov ni mmoja kati ya ndugu kumi nchini humo waliohukumiwa kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Saba walifungwa mwaka wa 2019 na watatu walifungwa mwaka wa 2018. Vifungo vyao ni vyenye urefu wa kati ya mwaka mmoja hadi miaka minne.
Ndugu Dovletov anaishi jijini Baýramaly, Mkoa wa Mary, kusini-mashariki mwa Turkmenistan. Anaishi na mke wake anayeitwa Surya, na mama yake anayeitwa, Sonya. Wote wawili ni Mashahidi wa Yehova pia.
Kesi ya Ndugu Dovletov ilianza kusikilizwa Novemba 11, 2019. Ndugu Dovletov alieleza mahakama kwamba anakataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri kwa msingi wa imani yake ya kidini. Kwa kuongezea, madaktari watatu walitoa ushahidi unaoonyesha kwamba Ndugu Dovletov ana vidonda ya tumbo vya kudumu kwenye utumbo mdogo, na kwa sababu hiyo anapaswa kupewa msamaha wa kutumikia jeshini.
Licha ya hayo, hakimu aliamua kwamba alikuwa na kosa la kutumia “ulaghai” ili kuepuka utumishi wa kijeshi hivyo akamhukumu afungwe. Inatazamiwa kwamba Ndugu Dovletov ataungana na wale ndugu wengine tisa waliofungwa katika kambi ya kazi ngumu ya Seydi iliyoko jangwani katika Mkoa wa Lebap. Ndugu Dovletov atakata rufaa hukumu hiyo.
Kadiri ndugu zetu nchini Turkmenistan wanavyoendelea kukabiliana na mateso, tunasali kwa ajili yao tukiwa na imani katika ahadi ya Yehova iliyoongozwa na roho kwamba atawategemeza kwa kudumisha utimilifu kwa ujasiri.—Zaburi 37:18, 24.

