AGOSTI 15, 2025
TAIWAN
Baadhi ya akina ndugu walioshiriki katika programu ya utumishi wa badala wa kiraia (ACS) kwa mara ya kwanza baada ya programu hiyo kuanzishwa huko Taiwan mwaka wa 2000
Miaka 25 ya Utumishi wa Badala wa Kiraia Huko Taiwan
Miaka 25 iliyopita, Serikali ya Taiwan ilianzisha utumishi wa badala wa kiraia (ACS). Programu hiyo inawapa wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri fursa ya kutumikia jamii. Wanatumikia jamii kwa kufanya kazi hospitalini, kwenye makao ya kuwatunzia wazee, na pia kwenye sehemu nyingine za umma. Zaidi ya ndugu zetu 1,000 wameshiriki katika programu hiyo tangu ilipoanzishwa.
Kabla ya mpango huo wa ACS kuanzishwa, ndugu vijana waliotimiza umri wa kwenda jeshini walifikishwa mahakamani na kisha kufungwa gerezani kwa sababu ya kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Baadhi ya ndugu hao walifungwa mara kadhaa. Lengo lilikuwa kuendelea kuwafunga gerezani hadi watakapofikisha umri ambao hawangetarajiwa kutumika jeshini.
Kupitia programu ya utumishi wa badala wa kiraia ndugu huko Taiwan hufanya kazi mbalimbali zinazonufaisha jamii
Ndugu Chengzhang Yang na mwana wake, Huadian, ambaye alikamilisha utumishi wa badala wa kiraia hivi karibuni
Ndugu Chengzhang Yang alifungwa gerezani kwa miaka minne kabla ya programu ya ACS kuanzishwa. Anasema hivi kuhusu hali nzuri iliyopo sasa: “Programu hii inawawezesha vijana ambao ni Mashahidi wa Yehova, kama mwanangu, kutimiza wajibu wao katika jamii na wakati uleule kutenda kupatana na imani yao. Tunathamini sana kuwa na mpango huu.”
Bw. Che-fang Shen, mkurugenzi mkuu wa Idara ya Usimamizi wa Usajili wa Utumishi wa Kijeshi
Hivi karibuni Bw. Che-fang Shen, mkurugenzi mkuu wa Idara ya Usimamizi wa Usajili wa Utumishi wa Kijeshi, alisema hivi: “Programu hii inaendeleza haki za kibinadamu na kulisaidia taifa na jamii pia na wakati uleule kuhakikisha kwamba kuna uhuru wa ibada. Ninaamini kila mtu anafaidika.”
Tunashukuru sana kwamba mpango wa ACS huko Taiwan unawawezesha ndugu zetu kutimiza wajibu wao katika jamii huku wakiendelea “kuutafuta kwanza Ufalme.”—Mathayo 6:33.

