Kiswahili
Baada ya Miaka 11, Mahakama Kuu Nchini Sri Lanka Yatoa Uamuzi Unaowaunga Mkono Mashahidi
https://cms-imgp.jw-cdn.org/img/p/702025113/univ/art/702025113_univ_sqr_xl.jpg

JULAI 18, 2025
SRI LANKA

Kushoto: Jengo la Mahakama Kuu ya Sri Lanka. Kulia (kuanzia kushoto kwenda kulia): Dada J.A.D.M. Malkanthi, Dada M.A. Suneetha Kalyani de Silva, Dada R.A. Niruja, na Dada Tisuri Ama Liyanage, mwezi Mei 2025

Baada ya Miaka 11, Mahakama Kuu Nchini Sri Lanka Yatoa Uamuzi Unaowaunga Mkono Mashahidi

Baada ya Miaka 11, Mahakama Kuu Nchini Sri Lanka Yatoa Uamuzi Unaowaunga Mkono Mashahidi

Mei 21, 2025, Mahakama Kuu nchini Sri Lanka ilitoa uamuzi muhimu ambao utawaruhusu watu wote nchini humo kuabudu kwa uhuru. Uamuzi huo ulitolewa miaka 11 baada ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa. Mahakama hiyo ilisema kwamba polisi walikiuka sheria na uhuru wa kuabudu walipowakamata dada zetu wanne. Uamuzi huu ni ushindi mkubwa wa kisheria kwa watu wa Yehova walio nchini Sri Lanka, kwa sababu kadhaa. Kwanza, unaunga mkono haki ya kisheria ya Mashahidi wa Yehova ya kuwaeleza wengine kuhusu imani yao kwa amani. Isitoshe, unaweka mfano mzuri wa kuheshimu uhuru wa ibada kotekote katika eneo la Kusini mwa Asia.

Oktoba 2014, dada zetu wanne walikuwa wakihubiri katika kijiji cha Kirama, kusini mwa Sri Lanka. Ghafla, kikundi cha watu wenye hasira kikaanza kujaribu kuwazuia Mashahidi hao. Polisi walipofika, waliwakamata dada hao wanne badala ya kuufukuza umati. Huo ulikuwa ukiukaji wa sheria. Waliwazuilia dada hao usiku kucha bila kuwasilisha mashtaka yoyote dhidi yao. Waliwaweka kwenye vyumba tofauti vya gereza vilivyokuwa na wahalifu wenye vurugu. Hata hivyo, dada hao waliendelea kumtegemea Yehova chini ya hali hizo na wakabaki wakiwa watulivu. Siku iliyofuata, dada hao waliachiliwa.

Mwezi mmoja baadaye, Novemba 2014, hakimu wa mahakama ya eneo hilo alitupilia mbali kesi hiyo bila kuisikiliza. Hata hivyo, dada hao walihisi kuwa haki zao za kibinadamu zilikuwa zimekiukwa. Hivyo, waliamua kutuma malalamishi kwa Tume ya Haki za Kibinadamu na kwa Mahakama Kuu ya Sri Lanka. Hatimaye, mwezi Mei 2025, Mahakama Kuu nchini Sri Lanka ilifikia mkataa kwamba haki za dada hao wanne zilikuwa zimekiukwa walipokamatwa, na ikaamuru mkuu wa Polisi wa eneo hilo pamoja na serikali kuwafidia kifedha dada hao. Dada Malkanthi anasema hivi kuhusu uamuzi huo wa Mahakama Kuu: “Uamuzi huu sio ushindi tu kwetu sisi wanne, bali unahakikisha kwamba haki ya kuabudu kwa amani ya ndugu na dada zetu nchini Sri Lanka inaheshimiwa. Mungu anaahidi kwenye Isaya 54:17 kwamba ‘hakuna silaha yoyote itakayotokezwa dhidi yako itakayofanikiwa.’ Ahadi hiyo imekuwa halisi zaidi kwangu sasa kuliko wakati mwingine wowote!”

Tunashangilia pamoja na ndugu na dada zetu nchini Sri Lanka kwa uamuzi huu unaotuunga mkono na unaohakikisha kwamba tuna haki ya kuendelea “kuishi kwa amani na utulivu na ujitoaji-kimungu kamili.”​—1 Timotheo 2:2.