Kiswahili
Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu Nchini Korea Imeomba Kuboreshwa kwa Utumishi wa Badala
https://cms-imgp.jw-cdn.org/img/p/702022065/univ/art/702022065_univ_sqr_xl.jpg

Wawakilishi wa Mashahidi wa Yehova wakikutana na msimamizi wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu Nchini Korea kuzungumzia utumishi wa badala wa kiraia. Baada ya mkutano huo, tume hiyo ilitoa taarifa rasmi kuhusu suala hilo

JANUARI 27, 2022
KOREA KUSINI

Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu Nchini Korea Imeomba Kuboreshwa kwa Utumishi wa Badala

Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu Nchini Korea Imeomba Kuboreshwa kwa Utumishi wa Badala

Ofisa wa haki za kibinadamu nchini Korea Kusini ametoa taarifa rasmi inayosema kwamba utumishi wa badala wa kiraia (ACS) nchini humo haupatani na viwango vya kimataifa vya haki za kibinadamu.

Desemba 2, 2021, Mwenyekiti Song Doo-hwan, ambaye ndiye msimamizi mpya wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu Nchini Korea (NHRCK), a alitoa taarifa rasmi kwenye tovuti yao kwamba matakwa ya ACS yanapaswa kubadilishwa. Korea Kusini ilianza mfumo wake wa ACS Oktoba 26, 2020.

Alisema hivi kwa sehemu: “Ingawa mfumo wa ACS ulianzishwa baada ya uamuzi wa Mahakama ya Kikatiba mnamo 2018, ninakubali kabisa kwamba kuna uhitaji wa kuboresha mfumo huo ili upatane na viwango vya kimataifa vya haki za kibinadamu . . .”

Taarifa hiyo ilitolewa Novemba 23, 2021 baada ya Bw. Song kukutana na wawakilishi wa ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova nchini Korea Kusini na wa Asia-Pacific Association of Jehovah’s Witnesses (APAJW). Ndugu hao walimpa Bw. Song ripoti yenye kichwa “Utumishi wa Badala wa Kiraia Nchini Korea Kusini—2021,” iliyotayarishwa na APAJW.

Ripoti hiyo inaeleza kwamba ACS nchini Korea Kusini inakiuka viwango vya kimataifa. Utumishi huo ambao unapaswa kufanywa kwa miezi 36 ni mara mbili ya utumishi wa kijeshi. Pia, utumishi huo wa ACS unadai mtu aishi katika hali sawa na za wafungwa. Kwa sasa wale waliokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri wanafanya kazi katika magereza. Wakati wa mwezi wao wa kwanza wa utumishi huo, hawaruhusiwi kuondoka katika eneo la gereza. Baada ya hapo, wanaweza kuondoka ikiwa tu watapewa idhini lakini wanapaswa kurudi kufikia saa 3:30 usiku.

Kwa sasa NHRCK inapitia maombi yaliyotolewa na wahusika wa ACS waliotuma maombi kwamba mfumo huo uboreshwe. NHRCK haina mamlaka yoyote ya kubadili sheria, lakini inaweza kutoa mapendekezo kwa ajili ya wanaotunga sheria.

Tunaimarishwa na imani na utimilifu ambao umeonyeshwa na ndugu zetu nchini Korea Kusini. Tunajua kwamba Yehova atawategemeza.​—Zaburi 55:22.

RIPOTI YA PEKEE: Utumishi wa Badala wa Kiraia Nchini Korea Kusini—2021

a NHRCK ni shirika la kutetea haki za kibinadamu lililoanzishwa mwaka wa 2001.