JULAI 18, 2019
ITALIA
Mahakama Kuu ya Italia Yalinda Haki ya Mashahidi wa Yehova ya Kupata Matibabu
Mei 15, 2019, Mahakama Kuu ya Italia, mahakama ya juu zaidi nchini, ilikazia haki ya ndugu zetu ya kujiamulia wenyewe juu ya matibabu wanayotaka. Mahakama hiyo ilithibitisha kwamba mgonjwa ana haki ya kujichagulia mwakilishi wake wa kitiba ambaye atatetea uamuzi wa mgonjwa wa kukataa kutiwa damu mishipani. Isitoshe, Mahakama hiyo ilisema kwamba sheria ya Italia inamruhusu mtu kuchagua mwakilishi wa kitiba atakayesimamia matibabu yake, na hilo linatia ndani pindi mgonjwa anaweza kupoteza fahamu ghafla au ikiwa afya yake inaweza kudhoofika kwa njia fulani.
Ndugu na Dada Cappelli
Uamuzi huo ulitolewa baada ya kusikilizwa kwa kesi kadhaa za Ndugu Luca Cappelli, ambaye ni mzee wa kutaniko. Amekuwa akisumbuliwa na ugonjwa mbaya unaoathiri neva za ubongo kwa miaka 25. Ndugu Cappelli anahitaji kutumia mbinu tofauti tofauti za matibabu na hata wakati mwingine tatizo hilo linaathiri uwezo wake wa kuwasiliana na watu. Kabla ya kuanza matibabu yake, alijaza kadi ya Uwakilishi wa Kitiba kwa kutegemea dhamiri yake, kisha akamchagua mke wake, Francesca, awe mwakilishi wake wa kitiba. Hata hivyo, hakimu na mahakama ya rufaa ilikataa kumteua mke wake kuwa mwakilishi wake wa kitiba, na hivyo kumnyima Ndugu Cappelli njia ya kujilinda kisheria ili asitiwe damu mishipani, jambo ambalo ni kinyume na mapenzi yake.
Kesi ya Ndugu Cappelli ilifika Mahakama Kuu ya Italia mnamo Februari 16, 2017. Mahakama Kuu ilikanusha uamuzi wa mahakama za chini zilizokiuka Katiba ya Italia na pia Mkataba wa Ulaya wa Haki za Kibinadamu zinazolinda haki ya mgonjwa kujiamulia mwenyewe. Jambo la kufurahisha ni kwamba Mahakama ilieleza kwamba kukataa matibabu fulani “kunahusisha hisia nyingi ambazo zinapaswa kulindwa kwa njia ya pekee, hasa ikiwa kukataa huko kunahusiana na imani ya kidini.” Kulingana na maamuzi haya ya Mahakama Kuu, mahakama za Italia zimesihiwa ziheshimu tahadhari ambazo ndugu zetu hufanya ili kuepuka kutiwa damu mishipani.
Familia yetu nzima yenye umoja inafurahi kwamba Mahakama Kuu imeamua kulinda haki za ndugu zetu wote nchini Italia, ambao wanaendelea kutii dhamiri zao zilizozoezwa na Biblia kuhusu matumizi ya damu.—Mdo 15:29.

