DESEMBA 31, 2019
CHILE
Mahakama ya Juu Nchini Chile Yatetea Haki za Mgonjwa
Desemba 13,2019, Mahakama Kuu nchini Chile iliamua kwamba mmoja wa Mashahidi wa Yehova alikuwa na haki ya kukataa kutiwa damu kwa sababu ya imani yake ya kidini. Uamuzi wa Mahakama Kuu ulibatilisha uamuzi uliofanywa na mahakama ya chini.
Dada Ríos akiwa na hati ya hukumu iliyofanyika Desemba 13, 2019
Kesi hiyo ilimhusu dada yetu, Polonia Ríos, ambaye alinyimwa huduma ya kufanyiwa upasuaji mara kadhaa kwa kuwa hakukubali kutiwa damu mishipani. Mwishowe alipeleka malalamiko yake dhidi ya hospitali hiyo ya serikali mahakamani. Agosti 6, 2019, Hospitali hiyo ilishinda kesi katika Mahakama ya Rufaa ya San Miguel.
Hivyo, Dada Ríos alikata rufaa kwenye Mahakama Kuu na kushinda kesi hiyo. Kwa mara ya kwanza Mahakama Kuu imetoa uamuzi unaolinda haki za watu wazima walio na uwezo wa kufanya maamuzi wanaokataa aina fulani ya matibabu kwa sababu ya imani zao. Kwa zaidi ya miaka 25, Mahakama iliamua kwamba mgonjwa hangeweza kukataa matibabu yoyote ambayo kulingana na maoni ya madaktari, yangeweza kuokoa uhai wake.
Uamuzi wa Mahakama unasema hivi, kwa sehemu: “Mshtaki . . . ni mgonjwa anayetamani kuishi na kufurahia afya njema baada ya kufanyiwa upasuaji ambao amekuwa akiusubiri kwa miaka mitatu . . . [Amekataa kutiwa damu mishipani] si kwa sababu zisizo na msingi, na si kwa sababu anataka kuwazuia madaktari wasimtibu. Bali uamuzi wake unategemea imani yake ambayo inapaswa kuheshimiwa kwa sababu ana haki kufanya uamuzi unaotegemea dhamiri na haki ya kutendewa kwa heshima. Tuna sababu nyingi zaidi za kuheshimu uamuzi wake kwa sababu ripoti zinaonyesha kwamba upasuaji huu unaweza kufanywa bila damu.”
Tunashangilia pamoja na ndugu zetu nchini Chile kwa ushindi huu unaofurahisha.—1 Wakorintho 12:26

