Kiswahili
Miaka 75 ya Kujenga Majumba ya Ufalme Nchini Afrika Kusini
https://cms-imgp.jw-cdn.org/img/p/702025130/univ/art/702025130_univ_sqr_xl.jpg

OKTOBA 2, 2025
AFRIKA KUSINI

Jumba la kwanza la Ufalme kujengwa nchini Afrika Kusini, lilijengwa jijini Cape Town, mwaka wa 1950

Miaka 75 ya Kujenga Majumba ya Ufalme Nchini Afrika Kusini

Miaka 75 ya Kujenga Majumba ya Ufalme Nchini Afrika Kusini

Mashahidi wa Yehova walijenga Jumba lao la kwanza la Ufalme nchini Afrika Kusini miaka 75 iliyopita. Tangu mwaka wa 1950, idadi ya wahubiri imekuwa ikiongezeka nchini humo. Hivyo, kazi ya kujenga na kudumisha Majumba ya Ufalme imeongezeka pia.

Majumba matatu ya Ufalme yaliyotumiwa na ndugu zetu katika miaka ya 1950

Kwa miaka mingi, ndugu na dada zetu walihitaji kukodi sehemu mbalimbali kwa ajili ya mikutano yao. Sehemu hizo hazikuwa na nafasi ya kutosha na hivyo ilikuwa vigumu kwa ndugu na dada kukazia fikira mikutanoni. Ndugu na dada wa kutaniko la Strand, Cape Town, walipopata pesa za kutosha, walianza kujenga Jumba la Ufalme la kwanza kabisa nchini Afrika Kusini. Akina ndugu walianza kujenga jumba hilo mwaka wa 1949, na likawekwa wakfu Septemba 17, 1950.

Kwa miaka 40 iliyofuata, ndugu na dada wengi walifurahia kutumia muda wao, pesa zao na ujuzi wao ili kusaidia katika kazi ya kujenga Majumba ya Ufalme kotekote nchini. Kisha katika miaka ya 1990, tengenezo la Yehova lilianzisha mpango mpya wa kujenga Majumba ya Ufalme haraka zaidi. Kwa mfano, Aprili 1992, Jumba la kwanza la Ufalme huko Diepkloof, Soweto, Afrika Kusini, lilijengwa kwa siku nne tu! Ujenzi wa Majumba ya Ufalme nchini Afrika Kusini uliongezeka zaidi baada ya programu ya kujenga Majumba ya Ufalme katika nchi zisizo na uwezo mkubwa wa kifedha, kuanzishwa katika mwaka wa 2008. Mpango huu uliwezesha tengenezo kutumia michango “ijazie uhitaji” katika nchi zisizo na uwezo mkubwa wa kifedha kwa ajili ya ujenzi wa Majumba ya Ufalme. (2 Wakorintho 8:14) Zaidi ya Majumba ya Ufalme 200 hivi yalijengwa nchini Afrika Kusini katika muda usiozidi miaka mitano. Majumba hayo yalitimiza uhitaji mkubwa kotekote nchini humo.

Baadhi ya Majumba ya Ufalme yaliyojengwa au kukarabatiwa kuanzia miaka ya 1990 mpaka leo

Katika mwaka wa 2014, programu ya Usanifu Majengo na Ujenzi (LDC) ilianzishwa ulimwenguni pote. Programu hii ilisaidia kuwazoeza ndugu na dada wengi zaidi, stadi mbalimbali za ujenzi. Chini ya programu ya LDC, Majumba ya Ufalme 250 hivi yamejengwa na mengine zaidi ya 800 yamefanyiwa ukarabati. Leo, kuna zaidi ya Majumba ya Ufalme 1,290 kotekote katika eneo la ofisi ya tawi ya Afrika Kusini.

Ndugu Buhlebakhe Mkhize, anayetumikia akiwa mwangalizi wa Idara ya LDC nchini Afrika Kusini, anasema hivi: “Tunafurahia kuona jinsi ambavyo Yehova anaharakisha kupanuka kwa ibada safi. Tunasali aendelee kubariki kazi ya ujenzi inayofanywa na ndugu na dada zetu nchini Afrika Kusini na ulimwenguni pote ili ilete utukufu kwa jina lake!”​—Zaburi 127:1.